Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo
akijiandikisha kwenye Orodha ya Daftari la Mpiga kura kwenye Kitongoji cha
Kimani Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani leo Tarehe 13.10.2019.
................................................
Na Oscar Job, Kisarawe.
WAZIRI wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameongeza siku tatu kwa wananchi
kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa
unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 Mwaka huu.
Akizungumza kabla ya kujiandikisha Kijijini kwake Kimani, Kisarawe
mkoani Pwani jana, Waziri Jafo alisema kuongezwa kwa siku tatu hizo kumetokana
na sababu mbalimbali ambazo kimsingi zimesababisha wananchi kuikosa fursa hiyo.
Alisema kimsingi siku za uandikishaji huo
zilizoongezwa kutoka leo hadi Oktoba 17, kumesabishwa na tatizo la mvua
zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali na hivyo kuleta shida kwa
wananchi wengi kujiandikisha.
Aliitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na uwepo wa
zoezi la wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, hali
iliyoleta dhana kwa baadhi ya wananchi kuwa kitambulisho cha mpiga kura
kitawawezesha kupiga kura katika uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.
“Kutokana na sababu hizo na kwa mujibu wa kanuni za
uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 na matangazo ya Serikali Na
371,372,373 na 374 ya Mwaka 2019 Waziri mwenye dhamana na Serikali za mitaa ana
mamlaka ya kutoa miongozo mbalimbali kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
alisema Jafo.
Alisema kutokana na kanuni hizo na changamoto
zilizojitokeza Wizara yake imeona vyema kuongeza siku hizo tatu ili kuwapa
nafasi wananchi kujiandikisha na hivyo kutumia fursa yao ya kikatiba kuwachagua
viongozi wanaowataka.
Aidha alisema tangu kuanza kwa Oktoba 8 hadi Octoba
12 Mwaka huu wananchi zaidi ya Milioni 11 walikuwa tayari wamejiandikisha nchi
nzima kushiriki uchaguzi huo huku akilitaja zoezi hilo kuwa lenye mafanikio
makubwa ikilinganishwa na kipindi kingine chote.
Alisema kufuatia mabadiliko, ratiba ya uandikishaji
wa orodha ya wapiga kura na matukio yanayohusu uandikishanji yatakuwa na
mabadiliko fulani fulani ikiwemo kubandikwa kwa orodha ya wapiga kura
litakalofanyika kuanzia Oktoba 18, utoaji wa pingamizi kuhusu uandikishaji
wapiga kura litakalofanyika Oktoba 14 hadi 24.
Mabadiliko mengine ni pamoja na uamuzi kuhusu
pingamizi litalofanyika kuanzia Oktoba 24 hadi 25,marekebisho ya orodha ya
wapiga kura kuanziaa Oktoba 25 hadi 25 pamoja na ukataji wa rufaa dhidi ya
uamuzi wa pingamizi utakaofanyika Oktoba 24 hadi 26 sambamba na ukataji wa
rufaa utakaofanyika Oktoba 24 hadi 29 Mwaka huu.
Aidha alisema matukio mengine yote zikiwemo kampeni
za wagombea zitaendelea kubaki kama kawaida huku akiwataka wananchi kuendelea
kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika uchaguzi
wa Serikali za Mitaa ili kuwa na sifa ya kupiga kura katika uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment