Monday, October 21, 2019

CHALINZE YAZINDUA CHANJO YA SURUA, RUBELLA

 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, akiwa amemshika mtoto anaechomwa sindano wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Surua, Rubella.
...............................

Na Athumani Shomari
Wananchi wilayani Bagamoyo wametakiwa kushiriki katika chanjo za kinga za magonjwa mbalimbali mara tu zinapotangazwa na serikali ili waweze kuendelea kuwa na afya imara kwaajili ya ujenzi wa taifa.


Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni alipokuwa akizindua kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua-rubela na polio za sindano katika Halmashauri ya Chalinze wilayani humo.


Alisema licha ya kuwepo Zahani, Vituo vya afya na Hospitali za wilaya, ambapo wananchi wanaweza kutibiwa, bado serikali imekuwa ikiandaa mipango ya kutoa chanjo za mara kwa mara zile zinazowalenga watoto na watu wazima ili kuwakinga na magonjwa ambayo yanaweza kuwadhoofisha.


Aliongeza kwa kusema kuwa, katika kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatangaza Tanzania ya viwanda iko haja pia ya kuimarisha afya za wananchi ili wawe na afya kwaajili ya kukabiliana na hiyo kasi ya viwanda.


"Kwa kuwa Rais wetu mpendwa, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli ameifanya Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda, hatuwezi kuwa na taifa la watu wenye maradhi na hasa ikizingatiwa kuwa, serikali inagharamia ili wananchi wake wapate chanjo hiyo" Alisema Bi Kasilda Mgeni.


Alisema wanachi wasiwafiche watoto wao katika mazoezi ya chanjo na badala yake kila wanaposikia kuna chanjo wanapaswa kujitokeza kuwapeleka watoto wao.


Aidha, alitoa wito kwa kina baba pia kutoa ushirikiano kwa kina mama katika kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya chanjo na kwamba kazi hiyo asiachiwe mama peke yake.


Awali akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, Mganga Mkuu wa Wilaya Chalinze (DMO) Dkt. Ernest Kyungu alisema walengwa wa chanjo ya Surua, Rubella ni 34,512 ambao kati yao waliochanjwa hadi kufikia oktoba 20, 2019, ni 28,456 sawa na asilimia 82.


Aidha, alisema walengwa wa chanjo ya Polio ya Sindano ni 14,646 ambao kati yao waliochanjwa ni hadi kufikia Oktoba 20, 2019 ni 13,861 sawa na asilimia 95.


Alisema zoezi hilo katika Halmashauri ya Chalinze limekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kupelekea baadhi ya vituo kuchelewa kuwafikia walengwa.


Hata hivyo, alisema timu ya uendeshaji wa huduma za afya ya wilaya imehakikisha shughuli zote zinatekelezwa kwa wakati kwa kufanya usimamizi shirikishi na kufuatilia maeneo yenye upungufu wa chanjo na vifaa vingine vya utekelezaji.


Kwa upande wake Diwani wa kata ya Msata ambae ni Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Selesitin Semiono, alisema anawashukuru wananchi wa Chalinze kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la chanjo.


Aidha aliwapongeza pia watumishi wa afya kwa kuendesha zoezi hilo katika mazingira magumu ya mvua ucheleweshaji wa malipo.


Diwani huyo alimueleza Katibu Tawala wa wilaya kuwa, wananchi wa Halmashauri ya Chalinze ni wepesi kuitikia matukio mbalimbali yanayotangazwa na serikali na hivyo kumtoa wasiwasi mgeni kuhusu kufikia lengo la Chanjo katika Halmashauri hiyo. 
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, (kushoto) akipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka (kulia) mara alipowasili katika Zahanati ya Msata kwaajili ya uzinduzi wa chanjo ya Surua . Rubella.
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, akielekea meza kuu mara baada ya kupokelewa alipowasili Zahanati ya Msata iliyopo Halmashauri ya Chalinze wilayani humo, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka na kulia ni Diwani wa kata ya Msata, Selestin Semiono.
 
Diwani wa kata ya Msata, Selestin Semiono, akiwakaribisha wageni katika uzinduzi huo, wa pili kulia ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka.
 
Mganga Mkuu wa Wilaya Chalinze (DMO) Dkt. Ernest Kyungu, (kushoto) akitoa taarifa ya chanjo katika Halmashauri ya Chalinze.
 
Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka, wakifuatilia kwa umakini taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Wilaya Chalinze (DMO) Dkt. Ernest Kyungu, wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Surua, Rubella, iliyofanyika katika Zahanati ya Msata.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Bi Amina Kiwanuka, akiwasalimia wananchi wakati wa kumkaribisha Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, ili aweze kuzungumza na wananchi.
 
Wananchi waliofika katika uzinduzi huo wakifuatilia hutuba za viongozi.

 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, akizungumza katika uzinduzi huo wa chanjo ya Surua, Rubella katika Zahanati ya msata.
  Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, akipiga picha na mtoto alifanyiwa uzinduzi wa Chanjo ya Surua, Rubella katika Zahanati ya Msata Halmashauri ya Chalinze.
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, (DAS) Bi Kasilda Mgeni, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Chalinze mara baada ya kuzindua chanjo ya Surua, Rubella.

PICHA ZOTE NA ATHUMANI SHOMARI. 

No comments:

Post a Comment