Na
Lillian Shirima–Maelezo
Imetimia miezi 48 sasa
sawa na miaka minne tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli alipochukua jukumu rasmi
la kuiongoza nchi Novemba 5, 2015.
Kiongozi huyu amefanikiwa
kuhakikisha watanzania wanatoka hatua moja kwenda nyingine kimaendeleo badala
ya kubaki kama walivyo miaka nenda miaka rudi. Aina ya uongozi wa rais Magufuli
umeonesha uwezo au karama ya kuondoa taratibu zilizooleka katika jamii na kisha
kubuni, kuelekeza njia sahihi kwa vitendo ni ushindi wa mafanikio katika
uongozi wake.
Katika kipindi kifupi
rais Magufuli amekuwa gumzo ndani na nje
ya nchi kutokana na uwezo alionao kushawishi
watu kufikia maendeleo yaliyotarajiwa kwa kuondoa taratibu zisizofaa kama vile uzembe kazini, ubadhirifu wa mali ya
umma, na huduma mbovu za jamii kama vile maji safi na salama, elimu, afya.
Akihojiwa na Idara ya Habari Maelezo mchambuzi na mtafiti wa wa masuala ya uchumi na siasa
“hakuna
jinsi nyingine kubwa ya kuhakikisha watu wanatoka hatua moja kwenda hatua
nyingine kama taratibu za maisha yao zinabaki zilivyo na tafsiri za kiuchumi
duniani zinaonesha kuwa maendeleo ya watu kiuchumi yanahusiana na utaratibu wa maisha ya watu
wenyewe, Rais wetu amevunja taratibu korofi ”. Anasema Dkt. Kahyoza.
Aidha, ameongeza kuwa kinachomtofautisha
rais Magufuli na viongozi wengine kiasi cha kusababisha awe gumzo ndani na nje
ya nchi ni muda mfupi aliotumia kuleta mageuzi makubwa nchini. Pia namna alivyoonesha mfano wa kubana matumizi
katika kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa nchi.
Mwandishi David Lender katika kitabu chake cha ‘The Wealth and Poverty of Nations: why some
are so rich and some are so poor (Utajiri na Umasikini wa Mataifa: kwanini mengine
ni tajiri na mengine masikini. Kitabu
hicho kimeeleza kwamba mataifa ambayo yameweza kuwa na sehemu kubwa ya
mabadiliko kati ya miaka 1961 na 2014 ni yale yaliyobadilisha taratibu na tabia za watu zilizooeleka
na kuzielekeza kwenda kwenye mtazamo wenye tija kwa taifa lao, miongoni mwa mataifa
hayo ni ulaya na Asia katika nchi za Uingereza, Japan na Afrika ni nchi za
Namibia, Botswana, Rwanda na Ethiopia.
Anasema, mfano hai ni kama vile uandaaji wa sherehe
za kitaifa za gharama kubwa, sherehe
wakati wa uteuzi wa viongozi mbalimbali, kumbukumbu za kitaifa, sherehe
za uhuru, muungano na uzinduzi wa miradi ambapo fedha nyingi hutumika
kusherehesha wakubwa serikalini na baadhi ya jamii.
Rais Magufuli alichukua hatua ya kubatilisha taratibu za
ufanyaji wa sherehe hizo kwa kufanya kazi za kijamii kama vile usafi, kuhudumia
wagonjwa na mara kadhaa kutumia fedha husika kwa ajili ya manufaa ya taifa ambapo
sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru aliagiza fedha zitumike kwenye
ujenzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco.
Pia, Rais Magufuli alipounda Baraza la Kwanza la Mawaziri 2015, Baraza lilikuwa
mawaziri 19 tu huku baadhi ya wizara zikibaki
bila naibu mawaziri. Rais aligiza kiasi cha shilingi bilioni 2 zilizokuwa zitumike
kwaajili ya semina elekezi kwa viongozi wapya zipelekwe Wizara ya Elimu
kutunisha fungu la elimu bure ikiwa ni pamoja na kununua madawati ya wanafunzi.
Rais hakuishia hapo, alizuia safari za viongozi nje
ya nchi zisizokuwa za lazima na yeye
mwenyewe kupunguza safari zake nyingi nje ya nchi na kuagiza balozi
kumwakilisha katika masuala ya Kimataifa.
Aidha, uzoefu wake katika kulitumikia taifa kwa
muda mrefu, aligundua ndani ya utumishi wa umma yapo makundi mawili ya
wafanyakazi wanaolipwa mshahara kwa mazoea. Kundi la kwanza ni watumishi ambao
kwenye kumbukumbu za utumishi wanaonekana waajiriwa wa serikali wanaolipwa stahiki zote za
utumishi lakini si watumishi ambao kwa
idadi walikuwa 20,000.
Kundi la pili ni watumishi ambao kwa mazoea
wanafanya kazi lakini hawana sifa kwa nafasi walizonazo kwa idadi walikuwa
14,000. Watumishi hao baadhi walitumia
vyeti visivyo sahihi kuajiriwa na wengine walifanya kazi za taaluma ambazo
hawakuwa na ujuzi nazo.
Kwa mamlaka aliyonayo, Rais Magufuli alitoa agizo
kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha watumishi
wa aina hiyo wanaondolewa sehemu zao za kazi. Zaidi ya watumishi 10,000
walipoteza ajira na serikali iliokoa zaidi ya shilingi Bilioni 15 za mishahara
hewa huku Wakuu wa Mikoa walioshindwa kutekeleza agizo hilo kwa usahihi
nyadhifa zao zilitenguliwa.
Pengine hali hii ndio iliyokuwa inasababisha hasira
dhidi ya serikali kwakuwa wananchi hawakuona huduma zinatolewa kama
zinavyostahili. Dkt. Kayhoza alisema kuwa nanukuu maneno ya rais Magufuli “Naagiza
wakuu wote wa mikoa hakikisheni watumishi hewa yaani ambao hawapo wanaondolewa
kwenye orodha ya utumishi na sehemu zao za kazi’.
Pia, matokeo yake ndani ya kipindi kifupi serikali
iliweza kutangaza nafasi za kwa wenye sifa katika sekta nyingi mathalani Tamisemi ilitangaza ajira mpya kwa walimu wa
shule za msingi na sekondari pamoja na sekta ya afya na nyingine nyingi.
Hii leo
watanzania tunaona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika utumishi wa umma.
Dkt. Kayhoza anasema, Rais Magufuli ameonyesha dhahiri
kuwa kiongozi bora asiye mlalamishi bali ni kiongozi anayetafuta ufumbuzi wa kila changamoto anayokutana nayo.
Aidha, ni kiongozi mwenye uthubutu , maamuzi sahihi, mtekelezaji, mfuatiliaji wa
maamuzi yake mpaka yanapokamilika.
“Hii
inaonesha dhahiri uwezo alionao wa kuzisoma nyakati na kuhakikisha nyakati hizi
zinaweza kutafsiriwa si tu kwa nchi anayoiongoza lakini pia kuangalia uchumi wa
nchi unategemea masuala gani yanatokea na namna gani yanaweza kusaidia nchi
kwenda mbele”. Amesema Dkt Kahyoza.
Maamuzi mengine aliyoyafanya ni serikali yake
kuhamia Dodoma. Hadi sasa Mawaziri wote chini ya Waziri Mkuu, Naibu Mawaziri,
Makatibu na Kurugenzi zote muhimu
zimehamia Dodoma.
Uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma haukupewa
kipaumbele kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita tangu ulipoasisiwa na Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye 1970. Kutokana na umuhimu wa
kuhamia Dodoma watumishi wa serikali waliokuwa makao makuu walihamia Dodoma. Hili ni funzo kwetu ambapo tukiamua tunaweza
kwani ndani ya matumizi na mazingira yetu ya kawaida inawezekana tukapanga na tukatekeleza
mambo yetu wenyewe kwa ufanisi.
Akitoa mfano juu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa
kufua umeme katika Mto Rufiji Dkt. Kahyoza amesema “Licha ya mradi huu utakaozalisha kilowati 2115 za umeme kupingwa na kukabiliwa na vizingiti ndani na nje ya nchi, Rais Magufuli ameweza kuvunja
vizingiti hivyo ambapo Julai mwaka huu alizindua rasmi ujenzi wa bwawa la mto
Rufiji utakaogharimu fedha za Tanzania za shilingi
trilioni 6.5.
Suala lingine ambalo rais Magufuli aliahidi kupambana nalo ni ukusanywaji
wa kodi ambapo ukaguzi kwa kila sekta umekuwa mkubwa na matokeo yake ni
kuongezeka kwa mapato ya taifa kutoka shilingi milioni mia nane kwa mwezi hadi
kufikia shilingi trilioni 1.7 Septemba, 2019.
Rais alisema“unapouza toa
risiti na unaponunua dai risiti”. Alianza
kwa kusisitiza kwa mtu mmoja mmoja kudai risiti kwa kila huduma anayopatiwa na baadaye akahimiza wafanyabiashara kulipa kodi ikiwa ni
pamoja na taasisi za serikali kulipa kodi baada ya kupatiwa huduma au bidhaa.
Hali hii imeleta mageuzi kwa kila mfanya biashara kuwa na mashine
ya EFD (Eletronic Fiscal Divice) kitu
ambacho hakijawahi kutokea miaka iliyopita. Amemalizia Dkt. Kayhoza
Naye
Projestus Rwegarulila Mkurugenzi wa Mradi wa Utamaduni na Uzalendo anasema,
Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiswahili kwenye
mikutano mbalimbali ya Kimataifa anayoshiriki jambo halijawahi kufanyika kwa viongozi wetu
hivi karibuni.
“Kitendo cha Rais kuongea Kiswahili kwenye
mikutano ya kimataifa kimewalazimu wasiojua lugha hiyo kutafsiriwa na wengine
kuamua kujifunza Kiswahili”. Anasema Rwegarulila.
Anasema,
pamoja na watu kuvutiwa na kile anachozungumza Rais kwenye mikutano, kasi ya
maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali ndiyo inawavuti wageni kuja
kujifunza namna ambavyo nchi imepiga hatua
kama vile mradi kama vile mwendo kasi, kuanzishwa kwa sera sera mpya ya
madini, ujenzi wa bwawa kubwa la
kuzalisha umeme ni baadhi ya baadhi ya mambo yanayoamsha kiu ya mataifa mengine
kujifunza kutoka kwetu.
Na
hakuna lugha nyingine isipokuwa kutafsiri Kiswahili katika lugha zao.
Naye
mwanafunzi Hamida Khamis wa shule ya msingi Bunge jijini Dar es Salaam amesema
kabla ya serikali ya awamu ya tano shule yao haikuwa na madawati ya kutosha,
wanafunzi walikuwa wanasukumana kutafuta nafasi za kukaa kwenye dawati lakini
mpango wa elimu bure umefanikisha shule kupata madawati ya kutosha.
Mkazi
wa Mugumu Serengeti Herman Peter yeye anasema, kabla Serikali ya Awamu ya Tano
kuingia madarakani huduma za afya zilipatikana katika Halmashauri ya Serengeti
tu lakini sasa huduma zimesogezwa karibu baada Serikali kujenga Kituo cha Afya katika
kata yao ya Nata kwa gharama ya shilingi milioni 400.
Nimalizie kwa kusema vema tukafahamu
Rais John Pombe Magufuli ameweza kuondoa taratibu zilizokuwa zikichelewesha nchi kusonga mbele. Hakuleta
sheria mpya au sera mpya, alichokifanya ni kuhakikisha yeyote anayepewa dhamana
ya uongozi anatimize wajibu wake, anaposhindwa
kuleta mabadiliko ndani ya muda mfupi anamwondoa
katika madaraka aliyokuwa nayo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
No comments:
Post a Comment