Friday, October 18, 2019

WAZEE TUNU YA TAIFA,TUWATUNZE- KIKWETE.

Na Shushu Joel

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Mh. Ridhiwani Kikwete amewataka vijana nchini kuwalinda, kuwatunza na kuwajali Wazee ambao ndiyo Walezi wa Jamii yetu.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na baadhi ya Wazee wa kata ya Bwilingu katika halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

"Wazee wamelipigania taifa hili , na sasa ni Muda muafaka wa sisi kupambana ili kulinda maslahi yao, wazee hawa walipambana sana kutufikisha tulipo, leo amani tunayoiona na maendeleo haya ni kazi waliyo asisi na hivyo juhudi zao zimetufanya sisi kuwa na amani kubwa na kuwa Mfano wa kuigwa na baadhi ya mataifa"Alisema Kikwete.

Aliongeza kuwa serikali ya Tanzania imejipanga ili kuhakikisha wazee wanaenziwa na kunufaika na nchi yao kutokana na kile walichokifanya wakati wa ujana wao.

Wamekuwa mstari wa mbele kushauri hivyo amewataka vijana kuongea na wazee mara kwa mara kwani wanaushauri mzuri juu ya mwenendo wa maisha yetu kama vijana.

"Vijana wengi tumeshindwa kujua na kutambua historia ya wazee wetu kutokana na kutokuwa karibu nao ili kujua jinsi wao walivyokuwa wakiishi na hivyo kujifunza toka kwao", Alisema.

Kwa upande wake Mzee Said Bwilingu (87) alisema kuwa amempongeza Mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete Kwa jinsi anavyowajali wazee Kwa kuwatembelea kila wakati na kuwajulia hali zao.

"Hivyo wazee tumefarijika sana kutembelewa na mjukuu wetu, sisi tuliishi na Wazee wake na hivyo Analolifanya mbunge ni kufuata mwenendo ulioasisiwa na wazee wake." Aliongeza kuwa amani ya nchi yetu inatokana na jinsi tulivyokuwa na umoja na mshikamano wenye nia ya kujenga taifa letu la Tanzania.


Wazee musiwatenge, Watembeleeni ili muweze kufaidika na mawazo yao japo vijana mnaona wa kizamani, alisema mzee huyo.

Aidha mzee huyo alisema kuwa anafarijika kuona jimbo la chalinze linavyozidi kupata maendeleo makubwa ambayo kipindi hicho ilikuwa ni historia lakini kwa sasa mambo mengi yanafanyika na kuleta neema kwa wananchi.

Pia amempongeza mbunge Ridhiwani Kikwete kwa ufanisi wake katika kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kwani wakati wetu maji, umeme, huduma za afya na miundombinu vilikuwa ni changamoto kubwa.

No comments:

Post a Comment