Friday, October 11, 2019

MKONGEA ATAKA UJENZI WA WODI YA WAZAZI NACHINGWEA UKAMILIKE HARAKA.

 
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mzee Ally Mkongea, akifungua kitambaa katika uwekaji wa jiwe la msingi jengo la wodi ya wazazi Hospitali ya Nachingwea.
............................................


Na Hadija Hassan, Lindi.


Wataalamu wanaotekeleza mradi wa Wodi ya kisasa ya Wazazi katika Hospital ya Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi wametakiwa kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakamilika kwa haraka ili wananchi waweze kutumia jengo hilo.


Wito huo umetolewa na kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mzee Ally Mkongea jana Oktoba 10 2019, alipokuwa anazungumza na wananchi pamoja na watumishi mbali mbali wa Halmashauri hiyo baada ya mbio za mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi katika mradi huo.


Mkongea alisema Serikali inapoamua kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa kama hiyo ina lengo la kuondoa kero kwa wananchi wake kwa kusogeza huduma Karibu na wananchi hivyo ni wajibu kwa wataalamu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.


Alisema ili kuharakisha ukamilishaji wa jengo hilo ni vyema kuweka oda ya Vifaa mapema wakati ujenzi huo unaendelea ili pia kuepuka kununua vifaa ambavyo sio imara kutokana na uharaka mtakaokuwa nao wa kutoa huduma mara baada ya jengo hilo kukamilika.


Pamoja na mambo mengine Mkongea aliwataka watumishi wa Hospital hiyo ya Wilaya kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma inayostahiki kwa kufuata Sheria na maadili ya kazi yao pamoja na kuwaasa wananchi kuacha kutumia tiba za kienyeji ambazo hazijathibitishwa na wataalamu.


Awali akisoma taarifa ya mradi huo Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Wilaya ya Nachingwea Dkt, Elias Zephania alisema mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia 'force Acount' kwa wakandarasi wa ndani ulianza 16/04/2019 na ulitakiwa kukamilika 16/08/2019.


Aidha kwa mujibu wa Taarifa ya Zephania inaeleza kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake utaghalimu kiasi cha shilingi milioni 431,919,430.88/= ambapo shilingi milioni 400,000,000/= zimetoka Serikali kuu na shilingi milioni 31,919,430.88/= kutoka Halmashauri ya Wilaya.


Alisema jengo hilo la Wodi ya wazazi litahusisha maeneo sita ambayo ni sehemu ya mama kusubiri kabla ya kujifungua, Sehemu ya kujifungulia , chumba cha upasuaji , sehemu ya waliojifungua bila upasuaji, sehemu ya waliojifungua kwa upasuaji pamoja na sehemu ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (njiti).


Zephania pia alieleza sababu za Mradi huo kuchelewa kukamilika kwa tarehe iliyopangwa kutokana na changamoto mbali mbali zikiwemo ugumu wa upatikanaji wa mafundi wenye uwezo kwa ajili ya kutekeleza mradi huo pamoja na kuchelewa kusoma kwa bakaa katika mfumo wa malipo wa FFARS baada ya mwaka mpya wa fedha kuanza.


Hata hivyo Zephania alibainisha kuwa ujenzi huo wa wodi utaongeza idadi ya wodi kwenye hospitali hiyo ambapo wodi ya wazazi iliyopo sasa itabadilishwa matumizi kuwa wodi ya watoto, huku wodi ya watoto ya sasa ikiwa wodi ya wanaume upasuaji ambayo awali haikuwapo kabisa.


Nae Mbunge wa jimbo hilo la Nachingwea Hasan Masala kwa niaba ya wananchi wa Wilaya hiyo aliishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuweka kipaumbele katika sekta ya Afya ambayo ndio msingi wa kaleta maendeleo kwa wananchi.


Masala alisema kuwa uwepo wa jengo hilo utaboresha huduma za mama na mtoto katika Hospital hiyo kwa kuwa na mazingira rafiki kwa mama kujifungu kwa njia ya kawaida na upasuaji.

No comments:

Post a Comment