Thursday, October 31, 2019

KAMISHNA MKUU TRA AWAPA NENO WAJUMBE WA KAMATI YA MAMLAKA ZA MAPATO AFRIKA MASHARIKI (EARATC) KUHUSU MAADILI

 
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, akisalimiana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Sudan ya kusini Bw. Erjok Geu, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 10 wa Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki (EARATC) kuhusu maadili unaofanyika jijini Dodoma.
......................................................
Na. Shushu Joel, Dodoma.

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hazinabudi kutilia mkazo suala la maadili ili kujenga uelewa wa pamoja na kuwa na mikakati shirikishi ya kutokomeza vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa mamlaka za mapato vinavyokwamisha ukusanyaji mzuri wa mapato.


Dkt. Mhede ameeleza hayo wakati akifungua mkutano wa 10 wa Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki (EARATC) kuhusu maadili unaoendelea Jijini Dodoma.

Amefafanua kwamba, katika mkutano huo masuala mbalimbali yanajadiliwa zikiwemo fursa mbalimbali pamoja na changamoto kama vile masuala ya upitishaji wa mapato haramu mipakani pamoja na namna ya kushirikiana katika kutoa adhabu kwa wafanyaji makosa hayo.

“Katika mkutano huu tunajadili masuala mbalimbali, mfano suala la maadili kama vile utovu wa nidhamu kwa watumishi wetu wa mamlaka za mapato, lakini pia tutaona namna ya kushirikishana katika kutoa adhabu kwa wafanyaji makosa katika upande mmoja aweze kudhibitiwa na upande mwingine”, alisema Dkt. Mhede.

Kwa upande wake, Mwenyekiti anayeongoza Mkutano huo, Dkt. Protazio Begumisa kutoka Uganda amesema kwamba, sababu inayowafanya kukutana mara mbili kila mwaka ni kukaa na kujadili na kuja na mikakati itakayosaidia kupambana na rushwa ili kuhakikisha kwamba inapungua ama inatokomezwa kabisa.

“Tunakutana mara mbili kila mwaka kwasababu sisi sote tunafahamu kwamba rushwa haiheshimu mipaka na tusipokuwa makini Wafanyabiashara wengi wataendeleza rushwa toka Dar es Salaam, Mombasa, Burundi hadi Rwanda kwani hawa watu wanatafuta mianya katika kazi zetu na endapo tukizubaa kidogo tunapoteza mapato’’, alisema Dkt. Begumisa.

Naye Katibu wa Kamati ya Mamlaka hizo za Mapato za Afrika Mashariki (EARATC), Bi. Esther Masibayi kutoka Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) ameeleza kuwa, katika Mamlaka za Mapato kupambana na rushwa ni jambo muhimu sana na suala la kukusanya kodi pia ni jambo muhimu, hivyo tunapokusanya kodi tujue kuwa kuna wengine wanakwepa kulipa kodi na kuendeleza vitendo hivyo viovu ndiyo maana lengo letu ni kuondoa hiyo tabia ya ukwepaji kodi ili tuongeze mapato katika Serikali zetu.

“Tunapopambana na rushwa lazima tukamate na tuwafunge watu, lakini hatuna magereza ya kutosha hivyo kikubwa ni kuwaelimisha ili wabadilike, ndiyo maana tunapaswa kubadili fikra zao ili waache kukwepa kodi na wakibadilika hii itawafanya wawe watu wema wenye kulipa kodi na Serikali zetu zitapata mapato ya kutosha’’, alisema Bi. Masibayi.

Mkutano wa 10 wa Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki kuhusu maadili (EARATC) hufanyika mara mbili kwa kila mwaka ukiwa na lengo la kujadiliana fursa mbalimbali pamoja na masuala ya maadili kwa watumishi wa Mamlaka za Mapato ikiwemo kupeana mikakati mbalimbali ya kuboresha utendaji katika kukusanya mapato ya serikali.

Sambambamba na hilo, mkutano huu hukutanisha jumla ya nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi pamoja Sudani ya Kusini.
 
 KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, akiwahutubia wajumbe wa mkutano wa 10 wa Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki (EARATC) kuhusu maadili unaofanyika jijini Dodoma.
 
 Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa 10 wa Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki (EARATC) kuhusu maadili unaofanyika jijini Dodoma wakimsikiliza KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede.

No comments:

Post a Comment