Tuesday, October 22, 2019

RC KAGERA ATOA SIKU TATU KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA BUKOBA KUHAMIA ENEO JIPYA LA MAKAO MAKUU YA WILAYA.

 Na Alodia Dominick, Bukoba.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametoa siku tatu kwa halmashauri ya wilaya ya Bukoba wawe wamehamia eneo jipya la makao makuu ya wilaya.

Brigedia Gaguti ametoa agizo hilo jana katika kikao cha kamati ya maendeleo ya mkoa kilichofanyika katika ukumbi mkuu wa mkoa wa Kagera ambapo pamoja na agizo hilo pia amesitisha mchakato uliofanywa na baraza la madiwani la kupendekeza eneo wapi makao makuu ya ofisi za wilaya hiyo zitajengwa.

Amesema, amesitisha mchakato huo kutokana na kwamba haukuwashirikisha wananchi badala yake walioshiriki walikuwa madiwani peke yao hivyo amesema mchakato huo inabidi uwashirikishe wadau mbalimbali ambao wako nje na ndani ya halmashauri ya wilaya ya Bukoba.

Awali kabla ya tamko la mkuu wa mkoa Octoba 16 mwaka huu baraza la madiwani la halmashauri hiyo lilikaa kikao maalum cha kupendekeza eneo litakalojengwa makao makuu ya halmashauri hiyo.

Maeneo yaliyokuwa yamependekezwa ni Bujunangoma katika kata ya Kemondo, Kyema na Rubale kata ya Rubale.


Baada ya vuta nikuvute kwenye kikao hicho mwenyekiti wa halmashauri hiyo Murshid Ngeze aliamua kutumia kanuni ya 28 ya kupiga kura za siri.

Kura zilipigwa na matokeo yalikuwa kama ifuatavyo, Kyema kura moja, Bujunangoma kura 22 na Rubale kura 16.

Hivyo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ngeze alitangaza kuwa, makao makuu yatajengwa Bujunangoma na halmashauri itahamia kemondo wakati wakisubili ujenzi wa ofisi za halmashauri.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameonyesha kutokubalianana maamuzi ya baraza hilo kwa madai kuwa eneo lililopendekezwa halijafuata wananchi.

Peter Kasiga mkazi wa kata ya Rubale halmashauri hiyo akiongea kwa niaba ya wananchi wenzake amesema, Rais Magufuli alikuwa na mtazamo mpana kwa sababu anapenda kuwahudumia wananchi wake na wapate huduma stahiki.

"Nafikiri kuna mambo hapa aliyoyaangalia na kuamua halmashauri zote zirudi karibu na wananchi, kinachonipa shida kwenye halmashauri yetu wamehama umbali wa kilomita saba kutoka mjini kitu ambacho hakiwezekani". Alisema Kasiga.

Alisema eneo stahiki la kuwa makao makuu ni Rubale pendekezo lililowahi kutolewa mwaka 2012 na 2013.

No comments:

Post a Comment