Friday, October 11, 2019

MBUNGE JUMAA KUJENGA UWANJA WA MPIRA MLANDIZI.

Na Omary Mngindo, Mlandizi

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijiji Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amesema kuwa atajenga uwanja wa Mpira wa Miguu wa kisasa mjini Mlandizi.

Jumaa ametoa kauli hiyo akiwa anazungumza na wakazi wa Kata ya Mtongani mjini hapa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake jimboni hapa, ambapo alisema hatua hiyo inalenga kuendelea kuupandisha hadhi mji wa Mlandizi.

Kauli ya Jumaa imefuatia swali la mmoja wa wakazi kuhoji mipango ya Halmashauri ya kutenga maeneo kwa ajili ya kuzikia, ambapo ofisa Ardhi Msaidizi Franck Mwalembe alimweleza Jumaa kuwa halmashauri tayari imeshatenga viwanja katika eneo la Kiwalani.

"Halmashauri imetenga eneo ya kuzikia, viwanja vya michezo na huduma mbalimbali za kijamii, niwatoe wasiwasi wananchi kuhusiana na maeneo muhimu, halmashauri yenu imejiandaa vizuri katika masuala ya kijamii," alisema Mwalembe.

Akizungumza na wananchi hao katika eneo la stendi ya Mtongani, Jumaa alisema kuwa pamoja naa kuwepo kwa uwanja wa Mpira wa Miguu wa JKT Ruvu uliopo maeneo ya Mlandizi Bondeni, nae atajenga mwingine ikiwa ni alama ya uongozi wake.


"Nimeamua kuweka alama kwa wananchi wangu wa Mlandizi, pamoja na kuwepo kwa uwanja wa JKT Ruvu nawahakikishia nitajenga uwanja wa Mpira wa Miguu, ili iwe kumbukumbu yangu kwa wana Mlandizi mlionichagua kuwaongoza kwa vipindi viwili vya ubunge wangu," alisema Jumaa.

Sanjali na hilo mbunge huyo amewataka wananchi jimboni humo kutokubali kuuza hovyo ardhi, kwani kwa sasa mji huo unakuwa kwa kasi kubwa, huku wawekezaji wakijitokeza kwa wingi kutaka ardhi kwa ajili ya kujenga viwanda vikubwa na vidogo.

No comments:

Post a Comment