Friday, October 11, 2019

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKABIDHI HUNDI YA MILIONI 127 KWA VIKUNDI LIWALE

Na Hadija Hassan, Lindi.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally amekabidhi hundi ya shilingi milioni 127,044,255 kwa vikundi 29 vya Wanawake, vijana na Watu wenye ulemavu Wilayani Liwale Mkoani Lindi.


Mkongea amekabidhi hundi hiyo katika kijiji cha Lindota Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mara baada ya kutembelea na kukagua shughuli mbali mbali zinazofanywa na makundi hayo ikiwemo vikundi vya ubanguaji wa Korosho, uchomeleaji vyuma, ukamuaji mafuta ya alizeti, ushonaji , Ufundi seremala pamoja na madereva Bodaboda .


Akizungumza na Wananchi pamoja na wajasiriamali hao Mkongea aliishauri Halmashauri hiyo kuangalia namna bora ya kuwasaidia wajasiriamali kuwakopesha mashine za kisasa ikiwa ni pamoja na zile za kubangulia korosho ili kufikia azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati na viwanda.


Hata hivyo Mkongea alisema kuwa ili vikundi hivyo viweze kuwa endelevu ni vyema kwa wajasiriamali hao wakaweka nguvu ya kuunganisha vikundi vyao ili Serikali iweze kuwakopesha vitendea kazi vitakavyoweza kuwarahisishia kazi zao.


Awali akitoa taarifa kwa kiongozi huyo wa Mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Liwale Mosesi Mkovele alisema fedha hizo za mikopo zimetokana na asilimia 10% ya makusanyo yao ya ndani ambayo ni ya awamu ya pili ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19 na awamu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2019/20.


Aidha Mkovele alibainisha kwamba shilingi milioni 58,488,219 zinazotolewa Zinakamilisha malipo kwa vikundi kutoka katika asilimia 10% ya mwaka wa fedha wa 2018/19 ambapo kwa awamu ya kwanza zilikuwa zimetolewa shilingi milioni 67,000,000 kati ya shilingi milioni 125,488,219 zilizopaswa kutolewa kama asilimia 10%.


Aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2019/20 Halmashauri hiyo imetenga kiasi cha shilingi milioni 202,180,860 ambapo kwa awamu ya kwanza jumla ya shilingi milioni 68,556,036 zinatolewa kwa vikundi husika. 

Kwa upande wake katibu wa mtandao wa vikundi vya wajasiriamali Wilaya ya Liwale, Mariamu Zuberi alisema kuwa Mikopo hiyo inayotolewa na Halmashauri itasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza kipato , kuongeza fursa za ajira, pamoja na kukuza mitaji kwa vikundi vinavyonufaika.

No comments:

Post a Comment