Monday, October 14, 2019

ZAIDI YA BILIONI 30 ZATUMIKA KUREKEBISHA MIUNDOMBINU KAGERA.

Katibu Tawala Mkoa wa Kagera (RAS) Profesa Faustine Kamuzora, akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya kupunguza maafa duniani.
.....................................................

Na Alodia Dominick, Bukoba.


Zaidi ya shilingi bilioni 30 zimetumika katika kurudisha hali na miundo mbinu iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea septemba 10 mwaka 2016 mkoani Kagera.


Takwimu hizo zimetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera (RAS) Profesa Faustine Kamuzora, wakati akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake juu ya siku ya maadhimisho ya siku ya kupunguza maafa duniani ambapo ameeleza kuwa, kwa kipindi cha takribani miaka mitatu iliyopita Mkoa wa Kagera umepata maafa ya tetemeko la ardhi lililosababisha miundo mbinu ya barabara na majengo kuharibika pamoja na vifo kwa wakazi wa mkoa huo.


Profesa Kamuzora ameongeza kuwa Kufuatia maafa hayo Serikali imekuwa ikijitahidi kurejesha hali ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 30 zimekwisha tumika Kwa kukarabati majengo ya Taasisi za serikali, Ujenzi wa Shule Mpya na miundo mbinu ya Barabara.


Ameendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya kukabiliana na maafa pindi yanapojitokeza, na tayari ipo kamati ya maafa inayohusisha Serikali, Taasisi binafsi na watu binafsi.


Kauli mbiu ya Siku hii Mwaka huu ni, "Chukua hatua endelevu kupunguza uharibifu wa maafa katika miundo mbinu muhimu na huduma za msingi ikiwemo afya na elimu, pamoja na kuimarisha ustahamilivu wake ifikapo 2030" ambapo Kitaifa Siku hii inaadhimishwa katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.


Oktoba 13 kila Mwaka Dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ambayo husababisha majanga mbalimbali na kupelekea athari vikiwemo vifo katika jamii husika.

No comments:

Post a Comment