Friday, October 11, 2019

Facebook yapanua mpango wa kutathmini usahihi wa taarifa zinazochapishwa hadi nchi 10 Kusini mwa Jangwa la Sahara



Nchi za Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, Cameroon, na Senegal ni miongoni mwa nchi ambazo zimejumuishwa katika mpango wa kuthibitisha taarifa zinazochapishwa kwenye mtandao wa Facebook uliotangazwa leo hadi kufikia nchi 10 barani Afrika. Mpango huu unatekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Agence France-Presse (AFP), France 24 Observers, Pesa Check na Dubawa, aidha mpango huu ni mkakati endelevu wa kupanua wigo wa kuthibitisha usahihi na ubora wa taarifa zinazochapishwa kwenye mtandao wa Facebook sambamba na kupunguza usambazaji wa taarifa za uongo kwenye mtandao huu.

Mpango huu unatekelezwa kwa ushirikiano na mtandao wa mashirika ya habari yanayothibitisha usahihi wa taarifa
yaliyoidhinishwa na Mtandao wa Kimataifa wa Kuthibitisha Taarifa usioegemea mrengo wowote, mpango huu wa uthibitisha taarifa zinazochapishwa utatekelezwa nchini Cote d’Ivoire, Ethiopia, Zambia, Somalia na Burkina Faso kupitia shirika la AFP,  nchini Uganda na Tanzania shirika la Pesa Check na AFP ndio watakaosimamia utekelezaji wa mpango huu, taarifa zinazochapishwa kwenye mtandao wa Facebook katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo zitathibitishwa na shirika la habari la France 24 na AFP huku nchini Guinea Conakry ikisimamiwa na shirika la habari la France 24, nchini Ghana taarifa zitathibitishwa na shirika la Dubawa.

Facebook inatumia kielelezo cha
maoni yanayotumwa na watumiaji wa Facebook kuainisha habari za uongo, taarifa hii hutumwa kwa mashirika mengine kuthibitisha usahihi wake. Taarifa, picha na video zote zinazochapishwa kwenye mtandao wa Facebook ndani ya nchi zitathibitishwa kuhakikisha kwamba ni za kweli. Mashirika tunayoshirikiana nayo kwenye mpango huu yakijiridhisha kwamba kuna habari ya uongo, Facebook itaweka habari hiyo sehemu ya chini ya Taarifa za Habari, kufanya hivi kutapunguza usambazaji wa taarifa husika.

Kojo Boakye, ni afisa Mkuu wa Sera ya Umma katika kampuni ya Facebook barani Afrika, anasema: “Kupanuliwa kwa wigo wa kuthibitisha habari na mashirika mengine hadi nchi 15 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ni ushahidi tosha kwamba Facebook imejitolea na kuweka kipau mbele barani Afrika, sambamba na kuongeza idadi ya lugha zinazotumika barani Afrika kama sehemu ya mpango huu. Tunafanya kila juhudi kutekeleza wajibu wetu wa kuchukua hatua madhubuti kupambana na habari za uongo zinazosambazwa kwenye mtandao wa Facebook, tunafahamu kwamba tatizo la habari za uongo limekuwa tatizo sugu, na mpango huu ni mkakati muhimu katika kutafutia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu. Tunafahamu kwamba kutumia Mashirika Mengine Kuthibitisha Taarifa hakutatua changamoto hii kabisa, lakini juhudi hii ni mojawapo ya mikakati na mipango tunayoendeleza ili kuimarisha ubora wa taarifa zinazopatikana kwenye mtandao wa Facebook. Ingawa tumepiga hatua kubwa, tutaendelea kuwekeza katika mipango ambayo itatuletea ufanisi utakaohakikisha kwamba Facebook inakuwa sehemu ambayo watumiaji wanapata habari zote, lakini sio kueneza habari za uongo.”

Mashirika ya Kuthitibisha Taarifa wanaposoma taarifa kuthibitisha ukweli wa habari husika, Facebook itaionyesha habari hiyo kwenye
Makala Yanayohusiana chini ya sehemu ya Taarifa za Habari. Wasimamizi wa Kurasa na watumiaji wa Facebook watapata arifa watakapojaribu kutuma habari au ikiwa tayari wametuma habari ambayo imethibitika kwamba ni uongo, kufanya hivyo kunawapa watu uwezo wa kujiamulia taarifa ambazo wangependa kusoma, kuziamini, na kutuma.

Kuhusu mpango wa kuthibitisha taarifa zinazochapishwa kwa lugha ya Kiingereza na Ufaransa  katika nchi nane barani Afrika Phil Chetwynd, Mkurugenzi wa Habari za Ulimwengu wa Shirika la AFP amesema:, “Usimamizi wa AFP una furaha kubwa kupanua wigo wa mpango wa kuthibitisha taarifa zinazochapishwa kwenye mitandao kwa ushirikiano na Facebook. AFP ina uzoefu wa muda murefu na sifa za ubora wa hali juu katika taaluma ya uanahabari barani Afrika na tutatumia mtandao wa mashirika na wanahabari wetu wabobezi katika bara hili kupambana na usambazaji wa habari za uongo.”

Eric Mugendi, Mhariri wa shirika la Pesa Check ambalo jukumu lake ni kuthibitisha taarifa zinazochapishwa kwa lugha ya Kiswahili ameongeza kwamba: “Mitandao ya jamii kama Facebook imebadilisha, sio tu vyanzo vya habari miongoni mwa Waafrika bali mitandao ya jamii imekuwa chanzo muhimu cha maudhui ya kidijitali au “intaneti” kwa Waafrika wengi. Kwa kiasi kikubwa mitandao ya jamii inaathiri mtazamo wetu wa ulimwengu, mijadala yetu ya umma na mahusiano yetu na watu maarufu katika jamii. Mradi huu ni mkakati utakaoleta ufanisi mkubwa katika kupanua mpango wa kuthibitisha taarifa ili kusahihisha taarifa ambazo zinaweza kuleta madhara hasi katika ulimwengu wa uhalisia. Muradi huu utatusaidia kukabiliana na habari za uongo moja kwa moja na kwa uharaka unaotakiwa. Kupitia muradi huu, tumeona matokeo chanya katika ushirikiano wetu na wachapishaji na umma kwa ujumla. Kadhalika muradi huu unawasaidia wataalam wetu wanaotathmini usahihi wa habari kufikia hadhira kubwa jambo ambalo halingewezekana bila muradi huu. Kwa kweli muradi huu umetusaidia sana kuelewa pengo lililopo na mambo mengine ambayo ndiyo mihimili inayosaidia kusambaza habari za uongo katika bara la Afrika. Mchango wetu unazidi kukua hatua kwa hatua ikiwa ni juhudi endelevu za kujenga jamii ya Afrika iliyohabarishwa sawa sawa.”

Akiunga mkono kujumuishwa kwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Guinea Conakry, na Cote d’Ivoire
Derek Thomson, Mhariri mkuu wa shirika la France 24 Observers, amesema: “Taarifa za uongo zimekuwa tatizo kubwa barani Afrika. Kila siku watumiaji wetu kutoka bara la Afrika wanatutumia picha na habari ambazo wanazipata kwenye mitandao ya jamii wakiuliza kama maudhui ya picha na taarifa hizo ni sahihi. Unaweza kuthibitisha? Ni wajibu wetu kama wanahabari kuhakikisha kwamba tunathibitisha taarifa zinazosambaa ili tutoe taarifa sahihi. Kushiriki kwetu katika mradi huu wa Facebook kunatusaidia kuhakikisha kwamba wale wanaotuma taarifa za uongo wanajua kwamba tuna ukweli na hawawezi kutupotosha”
Caroline Anipah, Afisa Mipango katika shirika la Dubawa (Ghana) ameongeza kusema: “Katika shirika la Dubawa tuna furaha kubwa kuona Ghana, nchi ambayo imekuwa mhanga na kushuhudia taarifa za uongo na uzushi zikienezwa kutokana na ufanisi wa teknolojia na kusambaa kwa intaneti, ikijumuishwa kwenye mpango huu. Dubawa imedhamiria kuimarisha ubora na usahihi wa habari zinazosomwa na umma kwa madhumuni ya kuzuia usambazaji wa habari za uongo na uzushi sambamba na kuendeleza utawala mzuri na kuhimiza uwajibikaji.”

No comments:

Post a Comment