Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii
na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Bi. Ruth Minja akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana Oktoba 8, 2019
wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba 2019 ambao
umeshuka hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka unaoishia mwezi
Agosti, 2019.
.....................................
Na Mwandishi Wetu
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa
mwezi septemba, 2019 umepungua hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa
mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa
Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja wakati akitangaza mfumuko wa bei hapo jana Tarehe 08 Oktoba 209
Jijini Dodoma.
“Kushuka kwa mfumuko wa bei
kunatokana na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha
mwezi Septemba 2019 ikilinganishwa na bei za kipindi cha Septemba,2018”.
Alisisitiza Bi. Minja.
Akifafanua amesema kuwa baadhi ya
bidhaa zilizopungua bei kwa mwezi Septemba ni mafuta ya taa asilimia 1.0,
Petroli asilimia 3.3 ,majiko ya gesi asilimia 1.5, dawa za kuulia wadudu
nyumbani asilimia 2.2 na mafuta ya nywele asilimia 1.3.
Aliongeza kuwa mfumuko wa Bei wa
bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019
umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi
Agosti, 2019.
Akizungumzia nchi za Afrika Mashariki
Bi. Minja amesema kuwa mfumuko wa Bei nchini Kenya kwa mwezi Septemba
umepungua hadi asilimia 3.83 kutoka 5.00 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti,
2019.
Kwa upande wa nchi ya Uganda, mfumuko
wa Bei kwa mwaka unaoishia mwezi Septemba 2019
umepungua hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka unaoishia mwezi
Agosti, 2019.
No comments:
Post a Comment