Na
Omary Mngindo, Kibiti.
WANAFUNZI
11 wanaosoma katika shule ya sekondari ya Kata ya Mjawa wilaya ya Kibiti mkoani
Pwani, wamepata mimba katika kipindi cha miaka miwili, kwa kuanzia 2018/2019.
Hayo
yamebainika katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Umoja wa Wanawake (UWT) mkoani
hapa mwishoni mwa wiki, ikiwa ni siku moja kabla ya kuhitimishwa kwa wiki ya
wanawake, ambayo kimkoa imefanyika wilayani Kibiti.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo Yusufu Mkupi ameuambia msafara huo ulioongozwa na Arafa
Kisera, Khatibu Chaurembo, Joyce Shauri, Josephine Gunda na Zaynabu Chitanda,
kuwa kwa mwaka 2018 wamepatikana wanafunzi watano waliopata mimba.
"Mwaka
2018 wanafunzi watano waliacha shule kwa ajili ya mimba, mwaka huu 2019 mwezi
wa pili wanafunzi wengine watano wamebainika wana ujauzito, na mwezi wa nne
tulipowapima amepatikana mwingine, hivyo kufanya wanafunzi 11 kukatisha masomi
kwa mimba katika miaka hii miwili," alisema Mkupi.
Mkupi
aliongeza kuwa sababu kubwa ya kushamiri kwa matukio hayo ni uhuru wanaopatiwa
wanafunzi hao, ambao wanaangalia video kwenye mabanda mpaka saa 5 au 6 usiku,
na wanaporejea majumbani hakuna mzazi anayemuuliza mtoto wake.
Akizungumza
na wanafunzi hao, Arafa Kisera amesikitishwa na hali hiyo, ambapo aliwaambia kuwa
matukio hayo ni ya aibu, na hasara kwao, huku akiwanyooshea kidole wanafunzi wa
kiume wanaojihusisha na vitendo vya kuingilia kinyume cha maumbile.
"Siku
hizi kumezuka tabia ya watoto wa kiume kuvaa nguo zao mlegezo, jiangalieni
msijihusishe na kuingiliana kinyume cha maumbile, vitendo hivyo ni hasara kwenu
hata mkija kuoa hamtakuwa na uwezo wa kuzalisha," alisema Kisera.
Kwa
upande wake Khatibu Chaurembo ambaye ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya
Kibiti, amewataka walimu hao kumpatia majina ya wanafunzi wote walioacha shule
kwa ajili ya mimba, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
"Hili
ndio kwanza nimelisikia hapa, walimu nipeni majina ya wanafunzi wote waliopata
mimba, tutakwenda kukaa na Kamati husika pamoja na viongozi mbalimbali, ili
kuhakikisha tunachukua hatua stahiki kwa walengwa," alisema Chaurembo.
Nae
Joyce Shauri, amewataka wanafunzi hao kutoona aibu kuwataja wanaojihusisha na
vitendo hivyo, huku akiwaambia kwamba kwa sasa mwanafunzi atakayebainika
kushika mimba yeye na aliyehusika wote wanashitakiwa.
No comments:
Post a Comment