Tuesday, October 29, 2019

TUWEKEZE KATIKA MAABARA - MSONDE

 
Mkurugenzi wa shule ya Sekondari Zamzam, Yahya Msonde, akizungumza katika mahafali hayo.
 
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, akizungumza katika mahafali hayo.
.................................................


Na Omary Mngindo.

WATANZANIA na Wadau wa elimu nchini, wetakiwa kujitolea kwa hali na mali kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa Maabara kwenye shule za sekondari, ili kuwapatia fursa wanafunzi kusomea sayansi.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa shule ya Zamzam Sekondari School iliyopo vijiji vya Kongo na Yombo wilayani Bagamoyo Pwani Yahya Msonde, katika mahafali ya kwanza shuleni hapo, mbele ya mgeni rasmi Mbunge wa jimbo hilo Dkt. Shukuru Kawambwa.

Akisoma taarifa yake mbele ya mgeni huyo aliyeambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ally Ally, Makamu Mohamed Usinga, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Fransic (Bolizozo) na waalikwa mbalimbali, Msonde alisema kuwa shule hiyo ina dhamira ya kuibua madaktari bingwa wa kike.

"Kwanza niwashukuru walimu wanaofundisha wanafunzi hapa shuleni, malengo makubwa ni kuwapatia fursa wanafunzi wa kike kuwa madaktari bingwa, kama ulivyoshuhudia onesho lao linavyolenga kupatikana kwa madaktari hao watakaosaidia katika upatikanaji huduma hususani kwa akinamama," alisema Msonde.

Akizungumzia changamoto zinazoikabiri shule hususani katika maabara, Msonde aliwaomba wazazi, walezi na wadau wote kujitokeza kusaidia upatikanaji wa vifaa kwenye Maabara, ili kuwezesha kupatikana madaktari wa kutosha wa kike.

Akizungumza na wahitimu hao pamoja na wazazi, Dkt. Kawambwa alianza kwa kumshukuri Mkurugenzi huyo kwa kumpatia fursa hiyo, huku akieleza furaha yake ya kuwa mgeni wa kwanza kwenye Mahafali, ambapo alisema wakati wa ufunguzi wa shule mwaka 2017 yeye ndie aliyefanya uzinduzu huo.

"Nakumbuka mwaka 2017 nilikuja hapa kulikuwa na hafla fupi ya ufunguzi wa shule, mabinti hawa wanaohitimu leo walikuwa wadogo sana, hatimae wamemaliza kidato cha nne, niwaase mkajiandae na mithihani ya taifa inayotaraji kufanyika hivi karibuni," alisema Dkt. Kawambwa.

Akijibia changamoto iliyopo katika Maabara, Dkt. Kawambwa amemhaidi Mkurugenzi huyo kwamba, atatafuta wahisani mbalimbali ili waweze kusaidia upatikanaji wa vifaa vitakavyosaidia wanafunzi kupata elimu ya sayansi.

Taarifa ya wahitimu iliyosomwa na Mwamahawa Mbilu na Bahiya imeelezea mafanikio yaliyopo shuleni hapo, sanjali na changamoto ikiwemo ya barabara, sekta ya afya sanjali na kutokuwepo kwa vifaa katika maabara ya shule.

No comments:

Post a Comment