Friday, October 25, 2019

TAG LAMKABIDHI MSHAMA MIFUKO 100 YA SARUJI


Na Omary Mngindo, Kibaha

KANISA la Tanzania Assemblies Of God (TAG) Jimbo la Pwani, limemkabidhi Mkuu wa wilaya ya Kibaha mkoani hapa Assumpter Mshama mifuko 100 ya saruji.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa ombi la Mkuu huyo kwa kanisa hilo, akilitaka limuunge mkono juhudi zake za kujenga vyumba 65 vya madarasa ikiwa ni kukabiliana na upungufu huo katika shule mbalimbali wilayani hapa, lengo ni kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi mifuko hiyo, Askofu wa Kanisa hilo Uswege Mwakisyala alisema kuwa baada ya kupokea ombi la kuunga mkono juhudi za uboreshaji elimu wilayani hapa, Waumini walikutana kujadiliana juu ya hilo, kisha kukubaliana kununua mifuko 100 ya sariji.

"Leo ninayo furaha kubwa mbele ya Waamini wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of Godd kwa lengo la kukukabidhi mifuko mia moja, hapa kanisani tunakukadidhi  mmoja, mingine ipo katika gari utatuelekeza eneo linalotakiwa ikashushwe," alisema Askofu Mwakisyala.

Mshama aliyeambatana na wajumbe wa Kamati Maalumu inayosimamia zoezi hilo iliyopewa jina la Elimisha Kibaha Mwalimu Joyce Shauri na Mwalimu Mohamed Mohamed, Mshama alianza kwa kuwashukuru Waamini hao kwa kuguswa na zoezi hilo.

"Tumezoea kuona watu wanachangia Kanisa, lakini kwenu mmeonesha moyo wa hali ya juu, katika kuunga mkono juhudi za ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa ili kukabiliana na upungufu uliopo," alisema Mshama.

Aliongeza kwa kusema kuwa baada ya kubaini upungufu huo alikuja na wazo hilo la kujenga vyumba vipya vya madarasa, ambapo alikitana na wadau mbalimbali ili wamuunge mkono, na kwamba zoezi hilo linakwenda vizuri.

"Tayari ujenzi wa vyumba hivyo umeshaanza katika maeneo mbalimbali, nitumie fursa hii kuwashukuru wote waliotuunga mkono, mkiwemo Waamini wa Kanisa hili la TAG," alimalizia Mshama.

No comments:

Post a Comment