Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameubeba
Mwenge wa Uhuru wakati aliposhiriki katika mapokezi ya Mwenge huo wilayani
Ruangwa yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu, Oktoba 9,
2019. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa na kushoto ni
Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Mzee Ali Mkongea.
Mwenge wa Uhuru umemaliza mbio zake leo Oktoba 10, 2019.
.............................
MWENGE wa Uhuru uliokuwa unakimbizwa
wilayani Ruangwa, mkoani Lindi umemaliza mbio zake na kukabidhiwa wilayani
Nachingwea.
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa,
Bw. Mzee Ali Mkongea amesema miradi mitatu ya maendeleo iliyopangwa kuzinduliwa
wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.
Miradi hiyo ni mabweni mawili kwenye
shule ye sekondari ya wasishana ya Hawa Mchopa, mradi wa maji wa Kitandi katika
kata ya Likunja na mradi wa barabara ya lami kwenye kata ya Nachingwea, iliyoko
Ruangwa mjini.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza
kupokea mwenge huo leo asubuhi (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) kwenye viwanja vya
shule ya msingi Chiola, wilayani Nachingwea, Bw. Mkongea amewataka wananchi wa
wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za
Mitaa na pia wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi huo, Novemba 24, mwaka
huu.
Mapema, akizungumza na wakazi
waliojitokeza kuupokea mwenge huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwenge
wa uhuru unakimbizwa maeneo mbalimbali nchini ili kuwahamasisha wananchi
washiriki kwenye shughuli za maendeleo.
“Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kwenye
maeneo yetu mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze kushiriki kwenye
miradi ya kujiletea maendeleo. Pia unaendana na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa
Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hivyo, tunakumbushwa kuyaenzi
mawazo yake,” alisema.
Mbali ya kuwahimiza washiriki
kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema kuna
makundi manne ambayo yanapaswa kushiriki uboreshaji wa taarifa zao kwenye
Daftari la Mpiga Kura pindi zoezi hilo likianza.
“Wanaotakiwa kushiriki zoezi hili, ni
wale waliopoteza vitambulisho vyao au wanavyo lakini vimefutika; waliohama
maeneo yao na wako kwenye maeneo mapya ambako watapigia kura mwakani; waliokuwa
na umri chini ya miaka 18 mwaka 2015 na sasa wamezidi umri huo; na wale ambao
mwakani wanatarajia kufikisha umri wa miaka 18,” alisema.
Mapema, akizungumza baada ya
kupokea mwenge huo saa 2:45 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Bi. Rukia
Muwango alisema leo utakimbizwa kwenye wilaya hiyo ambapo miradi yenye thamani
ya sh. milioni 781.5 itazinduliwa.
Kesho (Ijumaa, Oktoba 11) mwenge huo
utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na Jumapili (Oktoba 13)
utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14,
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment