Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana
Shonza, akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kufunga Tamasha la 38 la kimataifa la
sanaa na utamaduni lililofanyika TaSUBa mjini Bagamoyo.
.....................................
Wasanii
nchini wametakiwa kuboresha kazi zao ili ziingie kwenye ushindani wa soko ndani
na nje ya nchi.
Wito
huo umetolewa na Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana
Shonza alipokuwa akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 38 la kimataifa la
sanaa na utamaduni lililofanyika TaSUBa mjini Bagamoyo.
Alisema
kazi za sanaa na utamaduni ni miongoni mwa vitu vinavyokuza utalii hapa nchini
hivyo kazi hizo zinatakiwa kufanywa kwa umakini, ubunifu na utaalamu wa hali ya
juu ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko.
Aliongeza
kwa kusema kuwa, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa) ni chuo
chenye uzoefu wa kufundisha kazi za sanaa na uandaaji wa matamasha hivyo
wasanii watumie Tamasha hilo la mwaka huu kurekebisha kasoro zao walizoziona.
Alisema
wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kusimamia ubora wa
sanaa na utamaduni ili kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii, sana
iwe kivutio cha utalii hapa nchini.
Aidha,
Naibu waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa TaSUBa kwa
kuimarisha mahusiano mema kati ya Tanzania na nchi za nje kupitia sanaa na
utamaduni vinavyofundishwa chuoni hapo.
Alisema
kutokana na mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, wapo wanafunzi kutoka nchi
mbalimbali wanaokuja kusoma na pia wapo watanzania kupitia TaSUBa wanaenda
kusoma nchi za nje jambo ambalo linasaidia kukuza taaluma ya sanaa na
kuitangaza Tanzania kimataifa.
Alitoa
wito kwa uongozi wa TaSUBa mara tu baada ya kukamilika kwa tamasha hilo la 38
kukaa chini na kamati mbalimbali kutathmini namna lilivyofanikiwa tamasha la
mwaka huu ili kuboresha zaidi katika Tamasha la 39 litakalofanyika mwaka 2020.
Alisema
Tamasha la sanaa na utamaduni linatoa fursa kwa watanzania kufahamu kuwa kuna
watu wengi wenye vipaji na kwamba kupitia ubunifu mbalimbali unaofanywa na
wasanii, sanaa haiwezi kufa hapa nchini.
Aliongeza
kuwa, nje ya Tamasha huwezi kujua uwezo vipaji wa wasanii tofauti tofauti
lakini kupitia tamasha hilo vikundi mbalimbali vya sanaa na utamaduni vinaweza
kuwasilisha kazi zao na watanzania wakajionea wenyewe kwa muda wote wa siku
nane.
Awali
akizungumza mbele ya mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye alisema anaishukuru Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kushirikiana na Taasisi hiyo
ili kufanikisha matamasha yanayofanyika kila mwaka.
Alisema
Tamasha hilo ni muhimu sana ndani na nje ya nchini na kuiomba wizara hiyo,
iendelee kuliona tamasha hilo kama tukio muhimu kwa wizara katika kukuza na
kuendeleza vipaji vya wasanii hapa nchini.
Kwa
upande wake Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni, akizungumza wakati
wa kumkaribisha mgeni rasmi, alisema wilaya ya Bagamoyo inajivunia kuwepo kwa Tamasha
hilo licha ya kutangaza vipaji vya wasanii, pia linaitangaza wilaya ya hiyo,
Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla kwani linakuza mahusiano ya nchi mbalimbali
kutokana na wageni wanaofika kwenye tamasha hilo.
Alisema
miongoni mwa faida zinazopatikana katika tamasha hilo ni pamoja na kutoa ajira
kwa vijana na wajasiriamali.
Alimueleza
mgeni rasmi kuwa, kutokana na faida hizo zinazopatikana kwenye tamasha hilo,
wilaya ya Bagamoyo imehakikisha inaimarisha hali ya ulinzi na usalama ili
wageni wote waliofika wakae katika hali ya usalama.
Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, (katikati) akiwa katika sherehe za kufunga Tamasha la 38 la kimataifa la sanaa na utamaduni lililofanyika TaSUBa mjini Bagamoyo, jana Oktoba 26, 2019, kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya mambo ya kale, Dkt. Fabian Kigadye kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, wa pili ni Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya sanaa, kutoka wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joyce Fissoo na watatu ni Katibu Tawala Wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni, kutoka kushoto ni Mjumbe wa bodi ya ushauri TaSUBa, Lilian Godfrey Kihiyo, wapili ni
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye, akizungumza wakati wa kufunga Tamasha la 38 la kimataifa la sanaa na utamaduni lililofanyika TaSUBa mjini Bagamoyo, jana Oktoba 26, 2019.
No comments:
Post a Comment