Wednesday, October 23, 2019

TAKUKURU KAGERA YAWASHIKILIA WATUMISHI WANNE WA SERIKALI KWA TUHUMA ZA RUSHWA.

Na Alodia Dominick, Bukoba.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini, (TAKUKURU) Mkoani Kagera inawashikilia watumishi wanne wa Serikali katika matukio matatu tofauti ya kuomba na kupokea rushwa, wakiwemo Askari wawili mwanajeshi wa jeshi la wananchi (JWTZ ) na polisi.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera John Joseph, amesema wakiwa katika shughuli zao za kutekeleza majukumu yao Octoba 12 mwaka huu walipokea taarifa za tukio la Askari wa jeshi la Wananchi (JWTZ) koplo Nyambita Magoma mkufunzi katika ofisi ya mshauri wa Mgambo Wilaya ya Biharamulo, kukamata ng’ombe waliokuwa wameingia kwenye hifadhi ya Taifa (Biharamulo forest reserve) akaomba rushwa ya shilingi milioni 3 ili asimchukulie hatua.

Joseph, amesema uchunguzi wa TAKUKURU, ulibaini kuwa pamoja na kuomba kiasi hicho cha fedha Askari huyo alishikilia mifugo hadi alipopatiwa jumla ya shilingi laki 8 na kisha kumuachia mwananchi huyo aliyetoa taarifa takukuru.

Ameongeza taasisi hiyo inawashikilia watu wengine watatu ambao ni Askari polisi Koplo Nassoro Mirambo anayetuhumiwa kushirikiana na Asaph Manya kuomba na kupokea rushwa Agosti 23, mwaka huu 2019.


Manya akiwa muajiriwa halmashauri ya Biharamulo idara ya misitu aliomba shilingi laki 7 kutoka kwa mfanyabiashara wa Mkaa jina linahifadhiwa baada ya kukamata gunia 50 za mkaa.

Amesema TAKUKURU walibaini fedha hizo zilipokelewa Polisi na Nassoro Mirambo siku hiyo hiyo kwa mikupuo miwili kwanza laki 250,000 na mara ya pili alipokea shilingi laki moja na elfu arobaini na nane.

Aidha ameeleza, walipopokea kiasi hicho cha fedha walimrudishia mlalamikaji mkaa waliokuwa wanaushikilia jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Ameongeza pia wanamshikilia Afisa Afya wa Kijiji cha Nyakanazi wilayani Biharamulo Audastus Norbert kwa tuhuma za kuomba rushwa ya shilingi laki 2 na kisha kupokea kiasi cha shilingi elfu 50.

Amesema alipokea kwa mwananchi mmoja ili asimfungie bucha yake ya kuuza Nyama mara baada ya kumkuta na makosa akiwa katika shughuli za ukaguzi .

Aliongeza kuwa, uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote wanne watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.

No comments:

Post a Comment