Sunday, October 6, 2019

MIL. 200 KUNUNUA GARI ZA WAGONJWA CHALINZE

Na Omary Mngindo, Chalinze.

HALMASHAURI ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kununua magari mawili mapya ya kubeba wagonjwa maeneo mbalimbali.

Hatua hiyo imetokana na magari yake mawili kupata ajali, huku moja likiharibika ikiwa ni kati ya magari manne yaliyokuwa yanatoa huduma hiyo, yakipangwa kwa tarafa nne kati ya tano zilizopo ndani ya halmashauri hiyo.

Hayo yameelezwa na Mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni mjini hapa, ambapo alisema awali halmashauri ilinunua magari matatu, huku Rais Dkt. John Magufuli, akiwapatia moja na kuwa magari manne.

"Juzi nikiwa katika mkutano na wananchi pale Bwilingu, niliwaambia wananchi kwamba kikao cha fedha kilichokaa kwa kauli moja kimeidhinisha shilingi milioni 200, zitakazonunua magari mawili mapya, yatayobeba wagonjwa" alisema Ridhiwani.

Aidha mbunge huyo alisema kwamba katika hatua za haraka, tayari wamekubaliana kutoa moja ya gari kutoka ofisi ya Mkurugenzi, ili kusaidia upatikanaji wa huduma ya kusafirisha wagonjwa, huku wakisubiri magari hayo yatakayonunuliwa hivi karibuni.

Wakizungumza na Waandishi wa habari baada ya kikao hicho, wakazi wa Bwilingu wakijitambulisha kwa majina ya Samaha Juma, Mariamu Idd na Salama Salmini walishukuru hatua hiyo, huku wakisema kuwa walipopata taarifa ya ajali za magari hayo mawili walipatwa na mshituko.

"Binafsi naishukuru halmashauri yetu, chini ya Mbunge wetu Ridhiwani ambaue ametupatia habari njema za ununuzi wa magari mawili, kwani tulipopata taarifa za ajali za magari yetu tulipatwa na hofu kubwa kutokana na huduma tulizoanza kuzipata," alisema Samaha.

Halmashauri ya Chalinze iliyoanzishwa miaka minne iliyopita, imetenga bajeti ya mafuta kwa ajili ya gari za kubeba wagonjwa, hivyo hakuna mgonjwa anayetozwa fedha wakati anatolewa katika Zahanati, Kituo cha afya wala hospitali aliyepewa rufaha kwenda sehemu nyingine.

No comments:

Post a Comment