Wednesday, October 9, 2019

WANANCHI ELFU 83 BUKOBA WATARAJIWA KUJIANDIKISHA KWAAJILI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Aliyevaa suti nyeusi ni mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akikagua vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura serikali za mitaa.   Mkoa wa Kagera unatarajia kuandikisha wananchi milioni moja laki mbili na elfu themanini huku vituo vikiwa ni 3,738.
...............................


Na Alodia Dominick, Bukoba

Wananchi wa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wanaokadiliwa kuwa elfu themanini na tatu (83,000) wameanza kujiandikisha katika mitaa Yao kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa.

Msimamizi wa uchaguzi katika manispaa ya Bukoba Richardi Mihayo amesema kuwa, manispaa ya Bukoba inavyo vituo vya kujiandikisha vipatavyo 66 na wanatarajia wananchi 83,000 watajiandikisha katika zoezi hilo ambalo limeanza Octoba 08 na litaisha octoba 14 mwaka huu.

Akikagua baadhi ya vituo mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akiwa kituo cha Kabangamilembe kata ya Hamugembe manispaa ya Bukoba ametoa wito kwa wasimamizi wa vituo mbalimbali mkoani Kagera kuhakikisha wanaandikisha wananchi wa mitaa husika na siyo kufanya hujuma kwa kuwaandikisha wananchi ambao wanatoka vitongoji jirani.

Brigedia Gaguti ameongeza kuwa, sheria lazima ichukuliwe kwa wale watakaobainika wanajiandikisha kwenye vitongoji ambavyo siyo wakazi husika na kuwa wananchi wa mkoa wa Kagera wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye vitongoji vyao ili waweze kuwachagua viongozi wanaofaa katika uchaguzi huo unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Kabangamilembe kata ya Hamugembe manispaa ya Bukoba Zainabu Mugusha amesema katika kitongoji chake wananchi wanaendelea kufika kwenye kituo kujiandikisha ingawa wanakuja kwa kasi ndogo.

Mmoja wa waliokuja kujiandikisha katika kituo hicho Masoud Ibrahim amesema, zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura za serikali za mitaa baadhi ya wananchi wanalichangaya na zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupata kitambulisho cha mpiga kura katika uchaguzi mkuu mwaka kesho hivyo serikali inapaswa kutoa elimu kwa jamii ili wananchi watofautishe mazoezi hayo mawili.
 

No comments:

Post a Comment