Monday, October 14, 2019

APIGWA NA WAFUGAJI, APATA ULEMAVU NA MKE KADAI TALAKA.

Na Omary Mngindo, Kibiti.


JUMA Mwinyilaka (31) mkazi wa Kibiti Mkoa wa Pwani, amepatwa na ulemavu wa kudumu kufuati kupigwa mkuki mkononi na mgongoni na mfugaji aliyemtaja kwa jina la Ndingwa Nune Ndaki.


Mwinyilaka ambaye kwa sasa ana ulemavu unaosababisha kutoweza kufanya jambo lolote, umetokana na Ndaki aliyeingiza mifugo shambani kwake, ambapo wakati yeye na wenzake wakiiswaga kwenda ofisi ya Kijiji, mfugaji huyo akaanza kuwashambulia na mkuki.


Alisema kuwa wakiwa njiani kuelekea katika ofisi ya Kijiji umbali wa kilometa moja kutoka shamba, Ndakia akaanza kuwashambulia Nassoro na Fadhili Mchoro, alipotaka kuingilia ndipo akamchoma kwa mkuki mkononi na kiunoni.


"Baada ya tukio hilo nilipoteza fahamu, nikazindukia hospitali ya Mchukwi nikitibiwa, lakini kutokana na hali yangu kuwa mbaya nikahamishiwa Hospitali ya Muhimbili ambako nilikaa kwa miezi miwili," alisema Mwinyilaka.


Aliongeza kwamba kutokana na hali yake kuwa mbaya, mke wake alipoona hana uwezo wowote wa kufanyakazi za kilimo na za kujiingizia kipato, aliomba ampatie talaka ili akaolewe mbele.


"Nikawa sina budi nikaandika talaka nimkabidhi na hivi sasa ameshaolewa, lakini nimezaa nae, kwa sasa naomba msaada niweze kwenda nchini India nikatibiwe, nimeambiwa naweza kurudi katika hali yangu," alisema Mwinyilaka.


Mama yake Mwinyilaka Mauwa Mrisho alisema kuwa baada ya tukio hilo, alipigiwa simu na watu wakimweleza kuwa mtoto wake amepoteza maisha kutokana na kupigwa na wafugaji walioingiza mifugo katika shamba lake.


Aliongeza kuwa baadae akaambiwa kwamba hajafa, isipokuwa hali yake ni mbaya na kuwa amekimbizwa hospitali ya Mchukwi, kabla ya kupelekwa Muhimbili, kwa ajili ya matibabu zaidi.



Mkuu wa wilaya ya Kibiti Gulam Husein Shaabani Kifu alikiri kutokea kwa tatizo hilo, huku akisema kwamba sheria imechukua mkondo wake, ikiwa ni pamoja na mtuhumiwa kukaamatwa kisha kufikishwa Mahakamani na hukumu kutolewa.


"Mahakama imehukumu kutokana na sheria zinavyoongoza, hukumu imetolewa lakini mlalamikaji kama hajaridhishwa na hukumu hiyo ana haki ya kukata rufaa ngazi za juu," alisema Kifu.


Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kibiti Ally Ungando alielezea kusikitishwa kwake kufuatia tukio hilo na mengine yanayojitokeza, huku akiwataka wana-Kibiti kutokubali kuwapokea wafugaji wavamizi ambao ndio chanzo cha matukio hayo.

No comments:

Post a Comment