Sunday, October 13, 2019

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ARIDHISHWA NA MRADI WA MACHINJIO LINDI.

Na Hadija Hassan, Lindi.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ally aridhishwa na kasi ya Mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Manispaa ya Lindi Mkoani humo.


Mkongea ameyasema hayo  alipotembelea na kukagua katika mradi huo na kuona maendeleo yake Pamoja na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo pia mkongea ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kwa kuanzisha mradi mkubwa ambao utakuwa chanzo kizuri cha mapato katika Halmashauri yao.


Awali akisoma taarifa ya mradi huo Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Lindi Dkt. Iddi Nizar alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia mpango wa uendelezaji Miji na Manispaa Nchini (ULGSP) ambao kwa awamu ya kwanza unatekelezwa na mkandarasi M/S KINASHA BULDING CONSTRUCTION AND GENERAL SUPPLIES JV JECE LTD ya jijini Dar Es Salaam na kwamba utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.45.


Alisema Machinjio hayo kwa awamu ya kwanza yatahusisha Jengo la Machinjio, Nyumba ya mkaguzi wa nyama na kibanda cha mlinzi, ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha changalawe, milango mikuu na uzio wa kuzunguka machinjio na Sehemu ya kupumzikia mifugo huku awamu ya pili ikihusisha uwekaji wa vifaa kwa ajili ya kuchinja na kuchakata nyama.


Nae fundi mchundo wa kampuni hiyo Jafety Malima alisema kuwa mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wa awamu ya kwanza huku akitaja kazi zilizofanyika kuwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la machinjio kwa asilimia 95%, ujenzi wa nyumba ya mkaguzi na kibanda cha mlinzi kwa asilimia 95% na kwamba wanatarajia kuukabidhi kwa Halmashauri oktoba 28 mwaka huu.


Alizitaja kazi zingine kuwa ni Milango mikuu (mageti) na uzio 100%, sehemu ya kupumzikia wanyama asilimia 95% pamoja na miundombinu ya maji safi na salama kwa asilimia 95%.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga alisema kuwa mradi huo utakapokamilika utasaidia upatikanaji wa Nyama bora na salama kwa walaji wa ndani na nje ya mji wa Lindi, kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia tozo za uchinjaji na uchakataji wa nyama, kuongezeka kwa Fursa katika sekta ya mifugo hususani ufugaji, pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Manspaa ya Lindi .

No comments:

Post a Comment