Na
Alodia Dominick, Bukoba.
Taasisi
ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inatarajia kumfikisha mahakama ya
hakimu mkazi Bukoba, Kaimu meneja mkuu wa Ranchi za Taifa (NARCO) Profesa
Philemon Nyangi Wambura kwa tuhuma mbalimbali za rushwa ikiwemo kuomba shilingi
milioni 12,000,000.
Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera John
Joseph ameviambia vyombo vya habari kuwa, kaimu meneja mkuu wa NARCO
anatarajia kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa ikiwa ni pamoja na kuomba
na kupokea rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, ubadhilifu na uhujumu uchumi
kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa, sheria namba 11 ya mwaka
2007.
TAKUKURU
Mkoa wa Kagera ikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana
na rushwa mnamo septemba 23 mwaka huu ilipata taarifa kutoka kwa vyanzo vyake
ambavyo vilionyesha kuwa Profesa Wambura amekuwa akijihusisha na vitendo dhidi
ya rushwa ikiwemo kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya wafugaji wenye
uhitaji wa vitalu vya kufugia Ng'ombe au wenye vitalu ambao wanahitaji kuhuisha
mikataba yao ya awali.
Taarifa
ya uchunguzi imeonyesha kwamba Januari 3 mwaka 2018 profesa Wambura alipokea
shilingi milioni 12 kutoka kwa mtu mmoja ambaye jina limehifadhiwa kwa sababu
za kiuchunguzi ili aweze kumpatia kitalu kwa ajili ya kufanyia shughuli za
ufugaji huku akifahamu kuwa, jambo hilo ni kosa na kinyume cha sheria.
Aidha,
watu wengine wanne Octoba 25 mwaka huu walifikishwa mahakamani kwa tuhuma
mbalimbali ikiwemo kughushi na kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya
mwajiri.
Stanslaus
Katto ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule ya sekondari Kashenye
aliyefikishwa katika mahakama ya Hakimu mkazi Bukoba na kufunguliwa shauri
jinai namba 226/2019 kwa makosa ya kughushi, kujipatia mamlaka asiyokuwa nayo
na kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo kwa mkurugenzi wa halmashauri ya
wilaya ya Misenyi kwa lengo la kujipatia fedha kiasi cha shilingi 5.7 milioni.
Uchunguzi
uliweza kubaini kuwa, June 9 mwaka 2015 Kato alighushi sahihi ya mwenyekiti wa
serikali ya kijiji cha Bukwali na kisha kughushi sahihi ya mkandarasi wa
kampuni ambayo imehifadhiwa katika hati ya malipo iliyokuwa itumike kufanya
malipo kwa mkandarasi na kuwasilisha hati hiyo ya malipo kwa mkurugenzi wa
halmashauri ya Misenyi huku akifahamu kuwa jambo hilo ni kinyume cha sheria.
Watuhumiwa
wengine ni Richardi Machumi Kavogoro mwenyekiti wa kijiji cha Mkalinzi,
Josephati Desekahino Nzeye mtendaji wa kijiji cha Mkalinzi na Onesmo Mabadiliko
Tiara ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya vocher za pembejeo wa kata ya
Muganza kutoka halmashauri ya Ngara ambao walifunguliwa shauri la jinai namba
166/2019.
Wote
wamefikishwa mahakama ya wilaya ya Ngara octoba 25 mwaka huu kujibu tuhuma
zinazowakabili za kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
No comments:
Post a Comment