Friday, October 18, 2019

DC. JOKATE AWATAKA WANANCHI BAGAMOYO KUCHAGUA VIONGOZI WANAOENDANA NA KASI YA RAIS MAGUFULI

 
Kaimu Mkuu Wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akizungumza na wananchi wa kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo wakati alipotembelea halmashauri hiyo kuangalia hali halisi ya uandishaji wapiga kura ulivyofanyika.
.........................................
Na Shushu Joel.

Kaimu Mkuu Wilaya ya Bagamoyo, Jokate Mwegelo amewataka wananchi wilayani Bagamoyo kuwachagua viongozi wenye Utayari na Uwezo wa kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Wito huo ameutoa alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze kwenye viwanja vya kituo cha mabasi Cha Barabara ya Morogoro.

Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha na kuwasisitiza wananchi hao kutambua dhamana kubwa waliyonayo ya kuchagua kiongozi atakayekuwa ni kiungo kikubwa kwa viongozi wa juu na anayeweza kuendana na utendaji wa Rais Dkt. Magufuli.

"Jambo hili nimewatahadharisha mapema kabla ya kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwezi wa kumi na moja" Alisema DC Jokate.

Mbali na kuwahimiza Wananchi kujitokeza katika zoezi hilo Kaimu Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, amempongeza Mbunge wa jimbo la Chalinze Mh. Ridhiwani Kikwete kwa utekelezaji na ufanikishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo lake na juu ya yote alivyojitokeza yeye akishirikiana na wananchi kuhamasisha uandikishaji wapiga kura.

Hivyo amewataka wananchi hao kuwa na viongozi watakaochaguliwa katika vitongoji na vijiji wawe wachapakazi kama Mh. Mbunge na Mh. Rais wanavyoshirikiana kufanya kazi nzuri ya kuleta Maendeleo.

"Ninyi wenyewe Mashuhuda na Mbunge ameeleza jinsi Miradi mikubwa kama ya maji, afya, madarasa, miundombinu na umeme ilivyotekelezwa kwa asilimia kubwa sana, nakupongeza Mh. Mbunge kwa utekelezaji Mzuri wa majukumu yako, Alisema DC Jokate.

Naye mzee Zaidi Lufunga (78) akizungumza kwa niaba ya Wana Chalinze amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kujionea mafanikio makubwa yalifanywa na serikali ya awamu ya tano katika jimbo la chalinze.

"Miaka yetu changamoto zilikuwa nyingi sana lakini kipindi hiki cha Rais Magufuli kwa kushirikiana na mbunge wetu Ridhiwani Kikwete mafanikio tunayapata na kazi nzuri inaonekana, Alisema Mzee Lufunga.

Aidha amemuhakikishia Jokate kuwa, kwa hali hii ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na iliyokuwa ndio ndoto zao watachagua viongozi wenye hofu ya Mungu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa maslahi ya wananchi wote.


Kwa upande wake mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete amempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa ujio wake wa kujionea jinsi wana Chalinze walivyojitokeza katika zoezi la kujiandikisha kwaajili ya kupiga kura za viongozi wa serikali za mitaa na vijiji.


Aidha, amewapongeza wakazi wa kata ya Bwilingu kwa kujitokeza kwa wingi ili kumsikiliza mkuu huyo wa wilaya.

Mpaka kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura hapo jana Oktoba 17, Halmashauri ya Chalinze imefanikiwa kuandikisha  Asilimia 74 ya wananchi waliotarajiwa kujiandikisha.
  
Kaimu Mkuu Wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, alipofika kwenye moja ya vituo vya kuandikisha wapiga kura Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, pembeni yake mwenye kiremba ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni na mwenye fulana nyeupe ni Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao. 
Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya Jokate Mwegelo.
 
Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete (katikati) akimueleza Kaimu Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Jokate Mwegelo (kushoto) hali ya uandikishaji wapiga kura ilivyokuwa katika Halmashauri hiyo, katikati ya Mbunge na Mkuu wa wilaya ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni na kulia ni Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao.

No comments:

Post a Comment