Thursday, October 24, 2019

HALMASHAURI YA WILAYA BUKOBA YATEKELEZA AGIZO LA RC. KUHAMISHA MAKAO MAKUU YA WILAYA.

 
Ubao unaoonyesha makao makuu ya wilaya kama unavyoonekana ukihamishiwa makao makuu mapya ya muda kata ya Kemondo, wakati mchakato ukiendelea kujenga makao makuu ya kudumu ya halmashauri ya wilaya Bukoba.
 
Baadhi ya viti na meza vikihamishiwa makao makuu mapya ya muda kata ya Kemondo, wakati mchakato ukiendelea kujenga makao makuu ya kudumu ya halmashauri ya wilaya Bukoba.
.......................................................

Na Alodia Dominick, Bukoba

Halmashauri ya wilaya ya Bukoba imeanza kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa wa Kagera alilolitoa la kuwa wamehamia makao makuu ya wilaya hiyo ndani ya siku tatu.

Halmashauri hiyo imeanza kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa huo Brigedia jenerali Marco Gaguti alilolitoa octoba 21 mwaka huu katika kikao cha maendeleo ya mkoa (RCC) la kuhama mjini na kuhamia makao makuu mapya ya wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Bukoba Murshid Ngeze amesema, tayari wameanza kuhamia eneo la muda ambalo liko katika kata ya Kemondo wakati wakianza mchakato wa kuwatafuta wadau na kuwaandaa wananchi kwa ajili ya kukaa nao kupendekeza eneo yatakapojengwa majengo ya makao makuu ya wilaya hiyo.

Ngeze amesema kuwa, zoezi la kuhamia Kemondo limeanza octoba 22 mwaka huu ambapo wameanza na ofisi za mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF ni pamoja na kibao kinachoonyesha makao makuu ya wilaya hiyo.

“Kama halmashauri tumeanza kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa wetu alilolitoa katika kikao cha kamati ya maendeleo ya mkoa na tumehamisha ubao unaoonyesha makao makuu ya wilaya na ofisi za TASAF” Alisema Ngeze.

Ameongeza kuwa, wanaendelea kuhamisha idara moja baada ya nyingine hadi hapo watakapohakikisha wamemaliza kuhamisha idara zote.

No comments:

Post a Comment