Sunday, October 13, 2019

ZAIDI YA WANANCHI LAKI TANO KAGERA WAMEJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA KUPIGA KURA.

Na Alodia Dominick, Bukoba.

Wananchi wapatao 577, 330 Mkoani Kagera wameishajiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa huku halmashauri ya wilaya ya Bukoba ikiongoza kwa uandikishaji huo kwa asilimia 82.4 ikilinganishwa na wilaya nyingine za mkoa huo.

Takwimu hizo zimetolewa jana Oktoba 12, 2019. na mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti baada ya kufanya ukaguzi kwa baadhi ya vituo katika kata ya Kemondo na Maruku halmashauri ya wilaya ya Bukoba.

Brigedia Gaguti amesema, halmashauri ya wilaya ya Bukoba inaongoza kwa mkoa wa Kagera katika uandikishaji kwa ajili ya kupiga kura za serikali za mitaa kwa asilimia 82.4 ikilinganishwa na wilaya nyingine ambazo ziko chini ya asilimia 60 na kuwa wananchi waliokadiliwa kujiandikisha katika mkoa wa Kagera ni 1.2 milioni na ambao wameisha jiandikisha ni 577, 330.

Aidha amesema, watendaji wa kata na vijiji waendelee kutoa hamasa kwa wananchi ili siku  zilizobaki wananchi waweze kujitokeza kujiandikisha katika vitongoji na mitaa yao wapate haki ya kuwachagua viongozi wao.

Ameongeza kila mwananchi ahakikishe rafiki, jirani yake ndugu na jamaa wamejiandikisha katika maeneo yao na kuwa kwa kufanya hivyo watawapigia kura viongozi ambao ni waadilifu kutokana na siku za nyuma kuchaguliwa viongozi wasio na maadili ambao walishiriki kuuza ardhi za vijiji na hivyo kuwaletea hasara wananchi.

kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi mkoa wa Kagera, Mapinduzi Severian amesema kwamba, uandikishaji kwa ajili ya kupiga kura za serikali umeanza octoba 08 mwaka huu na utamalizika octoba 14 mwaka huu.

Naye Mtendaji wa kata ya Kemondo Syliacus Sostenes amesema kwamba, zoezi la uandikishaji katika kata yake halikwenda vizuri kutokana na zoezi hilo kuchanganywa na zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya mpiga kura.

No comments:

Post a Comment