Tuesday, October 22, 2019

WAZAZI BAGAMOYO WATAKIWA KUTHAMINI ELIMU BURE

Na Omary Mngindo, Lugoba.

WAZAZI wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wametakiwa kutumia fursa ya sera ya elimu bure, kuhakikisha watoto wanaenda shule, wanasoma na kuhitimu masomo yao kuanzia elimu ya msingi mpaka sekondari.

Akizungumza katika mahafali ya 28 ya kidato cha nne shule ya sekondari Lugoba, Mfanyabiashara Maarufu Subhash Patel alisema kwamba, licha ya kuwa elimu ya mtoto ni haki ya kikatiba, lakini pia fursa hii ya awamu ya tano itumike ipasavyo kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu.

Alisema kuwa akiwa Mfanyabiashara kiu yake kubwa ni kuona wilaya ya Bagamoyo inakuwa na wasomi wengi, watakaoweza kuhudumu katika nafasi mbalimbali vikiwemo viwanda vinavyojengwa kwa wingi ndani ya wilaya hiyo.

Patel aliyemwakilishi Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete, alisema kwamba sehemu ya mali anatumia katika kusaidia jamii katika masuala ya elimu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo na kuwasomesha wasiojiweza ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.


"Nimeamua kujenga mabweni katika sekondari ya Lugoba, miaka 18 iliyopita baada ya kuona watoto wanapanga mitaani, hatua iliyokuwa inawaweka katika hatari ya kupata mimba na magonjwa mengine," alisema Patel.

Taarifa ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Alhaj Abdallah Sakasa imeelezea mafanikio na changamoto ya upungufu wa mabweni mawili, hivyo amewaomba wadau kujitokeza kusaidia kuondoa tatizi hilo.

"Kwanza tukupongeze kwa hatua yako ya kuwa mlezi wa shule yetu, umeilea kwa miaka 14, umetujengea madarasa, mabweni, umechimba visima na shughuli nyingi za kimaendeleo ya shule yetu," ilieleza sehemu ya taarifa ya Sakasa.

Taarifa ya wanafunzi iliyosomwa na Maria Nducha na Mussa Khahindi walianza elimu ya sekondari mwaka 2016 na kuhitimu  2019 wakiwa 182, kati yao wasichana 96 wavulana 86.

No comments:

Post a Comment