Sunday, October 13, 2019

BAGAMOYO YAFIKIA ASILIMIA 55.12 UANDIKISHAJI WAPIGA KURA.

 
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard Kapinga (kulia) akielezea hali ya uandikishaji wapiga kura unavyoendelea wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipotembelea Kata za Halmashauri hiyo kuangalia zoezi hilo linavyoendelea, wa pili kulia ni
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi Fatuma latu.
........................................

Jumla ya wananchi 37,994 wamejiandikisha kwenye daftari la wapiga kura katika Halmashauri ya Bagamoyo mpaka kufikia tarehe 12 Oktoba 2019.


Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard Kapinga, alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ya Wialaya ya Bagamoyo wakati wa ukaguzi wa vituo vya kujiandikisha wapiga kura uliofanyika Halmashauri ya Bagamoyo.


Kapinga alisema jumla ya wananchi waliotarajiwa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwenye Halmashauri ya Bagamoyo ni 68,929 ambapo idadi hiyo ya waliojiandikisha kwa kipindi cha siku tano ni sawa na asilimia 55.12.


Alisema kutokana na hali hiyo, Halmashauri hiyo mpaka siku ya mwisho inaweza kufikia lengo la asilimia 100 katika kuandikisha wapiga kura.


Kamati ya Ulinizi na Usalama (KUU) ya Wilaya ya Bagamoyo imeongozwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Bi Kasilda Mgeni katika kukagua vituo vya uandikishaji wapiga kura katika kata mbalimbali za Halmashauri hiyo.


Akizungumza na wananchi katika vituo vilivyotembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura ili kila mwananchi apate haki yake ya kupiga kura siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mita, Vitongoji na Vijiji ambayo inatarajiwa kuwa ni Novemba 24, 2019.


Alisema kuchagua viongozi ni haki kila mwananchi aliyefikisha umri wa kupiga kura hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuitumia haki hiyo ili kuchagua viongozi watakaofaa kuongoza na kuleta maendeleo.


Alisema katika kipindi hiki wapo baadhi ya watu ambao wanapita kuwadanganya wananchi kuwa hakuna umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ambapo amewataka wananchi hao kuacha kudanganywa na kwamba kila mwananchi atumie nafasi hiyo vizuri kwa maslahi yake, familia yake, eneo lake analoiishi na Taifa kwa ujumla.


Katibu Tawala huyo wa wilaya alisema Serikali ya wilaya ya Bagamoyo haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakaebainika kuhujumu uchaguzi huo kwa maslahi yake binafsi.


Alisema maendeleo katika ngazi mbalimbali yanaletwa kwa kusimamiwa vizuri na viongozi, hivyo ili kupata viongozi hao ni lazima wananchi wafuate taratibu za kupiga kura ikiwemo kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.


Aliongeza kwa kusema kuwa, katika kipindi hiki wananchi wasikubali kudanganywa na kuchagua watu ambao hawana uchungu wa maendeleo na badala yake wachague viongozi waadilifu, wenye maono ya maendeleo, na watakaofanya kazi kwa kujituma ili kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.


Aidha, alimalizia kwa kufafanua kuwa, ili mtu apate haki ya kupiga kura siku ya uchaguzi, njia pekee ni kujiandikisha kwenye daftari na si vinginevyo.


Alisema kitambulisho cha mpiga kura, kitambulisho cha uraia havitamuwezesha kupiga kura hivyo waisiache kujiandikisha kwa kudhani wanaweza kupiga kura kwa kutumia kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura.


Kwa upande wake Kamanda wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo, Raymond  Katima, amewataka wananchi wilayani hapa kujiepusha na vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na Vijiji.


Katima alisema kila mwananchi anayo haki ya kumchagua kiongozi amtakae na kwamba asikubali kupewa kitu cha aina yoyote kutoka kwa mgombea ili amchague kwani kufanya hivyo atakuwa amepokea rushwa na kuuza uhuru wake wa kumchagua kiongozi.


Alisema katika kipindi hiki wapo baadhi ya wagombea wanatamuia mbinu mbalimbali ili kupata madaraka ikiwemo kutoa rushwa, na kuonya kuwa, atakaebainika kutoa au kupokea rushwa ya aina yoyoyte hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


Alisema wananchi wasikubali urafiki wa muda mfupi wenye lengo la kubadilisha mawazo yao katika kuchagua viongozi.


Halmashauri ya Bagamoyo ina jumla ya kata 11 ambazo ni Yombo, Fukayosi, Zinga, Kerege, Mapinga, Kiromo, Dunda, Magomeni, Nianjema, Kisutu na Makurunge.
  Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni (kulia) akichukua taarifa za uandikishaji wapiga kura kwenye kituo cha uandikishaji wapiga kura Mwavi kata ya Fukayosi Halamshauri ya Bagamoyo, katikati ni
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard Kapinga.
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni akichukua taarifa za uandikishaji wapiga kura kwenye kituo cha uandikishaji wapiga kura, Kitongoji cha Kibaoni kata ya Makurunge katika Halmashauri ya Bagamoyo.
 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni akionyesha kitambulisho cha mpiga kura na kuwafahamisha wananchi kwamba kuwa nacho hicho hakumfanyi mtu kupiga kura bila ya kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bi Fatuma Latu.
 
Wananchi wakimsikiliza Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika kituo cha Mwavi kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo.

 
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika kijiji cha Kongo kilichopo kata ya Yombo Halmashauri ya Bagamoyo wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) ilipotembelea vituo vya kujiandikisha wapiga kura.
Wananchi wakimsikiliza Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika Kitongoji cha kifude kata ya Makurunge, halmashauri ya Bagamoyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bi Fatuma Latu, (kushoto) akisalimia wananchi wa Kitongoji cha Geza ulole kata ya Makurunge pamoja na kumkaribisha Katibu Tawala (DAS) wilaya ya Bagamoyo ili azungumze nao. waliokaa wa pili kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, anaefuata ni Afisa, Tarafa Tarafa ya Mwambao Dorisi Mwakatobe na wa kwanza kulia ni Afisa Tarafa, Tarafa ya Yombo, Gladness Shafii.
Wananchi wakimsikiliza Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, katika Kitongoji cha Geza ulole, kata ya Makurunge, halmashauri ya Bagamoyo. 
Kamanda wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo, Raymond  Katima, ambae ni Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, (KUU) akizungumza na wananchi kuhusu madhara ya rushwa wakati wa kukagua vituo vya kuandikisha wapiga kura.   
Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Kasilda Mgeni, (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bi Fatuma Latu, wakimsikiliza Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo alipokuwa akitoa elimu ya rushwa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment