Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu( wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kuzindua na kuwasha umeme katika
moja ya nyumba za Kijiji cha Mpiji katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kibaha, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Amour Jumaa, na wapili
kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama.
.......................................
Na Zuena Msuya , Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kutoa taarifa za
utekelezaji wa Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini kwa viongozi wa vijiji
pamoja na wananchi wa maeneo husika ili wafahamu hatua zaidi za utekelezaji wa
miradi hiyo.
Mgalu alisema hayo kwa nyakati
tofauti, Oktoba 16, 2019 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuzindua na kuwasha
Umeme katika Kijiji cha Mpiji, Kata Boko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha,
mkoani Pwani na kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji Umeme katika vijiji
vya Kiluvya, Misugusugu, Mkombozi pamoja na katika Mtaa wa Mwambisi wilayani
humo.
Aidha Mgalu alisema, kuwa TANESCO
wakiweka utaratibu wa kuzungumza na Viongozi wa Vijiji pamoja na wananchi mara
kwa mara juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi husika, kutaondoa
maswali mengi pamoja na wasiwasi walionao wananchi dhidi ya utekelezaji
wa miradi ya maendeleo hasa usambazaji wa umeme.
“Unajua watanzania ni waelewa sana, unapompa
mtu taarifa ya kile kinachofanyika katika eneo lake kwa wakati sahihi inamfanya
awe na amani na wale waliopewa dhamana ya kutekeleza jambo husika, pia
kuendelea kuiamini serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
kwa wananchi wake, na hii itawaondolea hofu na maswali mengi wananchi,
sasa msipofanya hivyo, wao watajuaje kinachoendelea katika maeneo yao!? Tanesco
waelezeni wananchi kila hatua inayofikiwa katika kutekeleza miradi ya umeme”,
alisisitiza Mgalu.
Vilevile alitumia ziara hiyo
kuwaeleza watanzania ambao bado hawajafikiwa na miradi ya usambazaji wa
umeme kuwa na subira wakati serikali inaendelea kutekeleza kazi hiyo kwa
awamu, kwa kuwa si jambo jepesi kuwafikia wananchi wote kwa siku moja.
Aliweka wazi kuwa lengo la serikali
ni kufikisha huduma ya umeme kwa kila mtanzania, na kueleza kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Vijiji 2018 tu, ndiyo vilivyokuwa na umeme,
sasa hivi idadi imeongezeka na kufikia zaidi ya vijiji 8100 na tayari zaidi ya
vijiji 6000 vimeunganishwa, lengo ni kuvifikia vijiji vyote 12,319 nchi nzima
ikifikapo mwezi Juni ,2021.
“ Serikali ya Awamu ya Tano
inatekeleza miradi mingi na muhimu katika kila sekta, kuna miradi ya Afya,
Elimu, Barabara, Maji na kadhalika, hii yote inahitaji fedha nyingi na iwafikie
wananchi wote na kwa wakati, serikali yetu ni sikivu na inatekeleza haya yote
kwa wananchi wake, hivyo fedha inayopatikana inagawanywa katika kila sekta ili
kutekeleza huduma zote muhimu kwa awamu kadri fedha inavyopatikana, hivyo wale
ambao bado hamjafikiwa kuweni na subira, lengo ni kuwapatia wananchi wote
huduma bora”, alisema Mgalu.
Mgalu alieleza kuwa, mkandarasi wa
kampuni ya Sengerema amefikia 90% ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme
katika vijijini vyote vya Wilaya ya Kibaha, kazi kubwa aliyonayo sasa ni
kuwasha vijiji hivyo hadi mwezi Desemba 2019, kisha kuangalia mapungufu yalipo
na kuyafanyia kazi, ili ifikapo mwezi Juni 2020 awe amemaliza mradi huo na
kuukamilisha kwa wakati.
Aliendelea kumsihi mkandarasi huyo
kuongeza kasi ya kuwaunganisha wateja ambao tayari wamelipia huduma hiyo,
sambamba na hilo aliwahimiza wananchi kulipia haraka gharama za kuunganishiwa
umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu.
Serikali ilitenga zaidi ya shilingi
Bilioni 17, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme
Vijijini katika Mkoa wa Pwani, pia iliongeza shilingi Bilioni 14 kwa
ajili ya utekelezaji wa Mradi wa
Usambazaji Umeme katika Vijiji vilivyopo Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban) katika Wilaya ya Kibaha pekee,
vilevile kupitia mapato ya ndani ya TANESCO, miradi ya usambazaji umeme 11
itatekelezwa katika wilaya hiyo kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa
ya umeme katika wilaya hiyo yanayosababishwa na uwepo wa viwanda.
Aidha katika mazungumzo yake na
wakazi wa Kijiji cha Misugusugu, aliitaka TANESCO kuwafungia Transfoma
inayokidhi mahitaji ya umeme katika kijiji hicho na maeneo yanayowazunguka ili
kuondoa adha ya kukatika umeme katika eneo hilo mara kwa mara ambayo
inasababishwa na kuelemewa kwa transfoma iliyopo.
Hata hivyo aliwaagiza watendaji wa
TANESCO kufanya uchunguzi upya kubaini kaya za maeneo ya kijiji cha
Misugusugu zilizoachwa katika awamu zilizotangulia ili na wao wapate
umeme katika awamu zijazo kwa kuwa zoezi la kusambaza umeme vijijini na
kuwaunganisha wateja ni endelevu kwa kuwa kila siku mahitaji ya umeme
yanaongezeka nchini.
No comments:
Post a Comment