Wednesday, October 9, 2019

KIKWETE ATAKA VIONGOZI KUSIKILIZA MAWAZO YA WATU WAO.

 Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akizungumza wakati akizindua Kongamano la Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere. Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere limefanyika leo katika Chuo hicho na kuhudhuria na  watu wa kada mbalimbali.
....................................


Na Said Mwishehe.

RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete amesema kuna kila sababu ya Watanzania kuendeleza misingi imara iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere huku akisisitiza umuhimu wa watu kuwa huru kutoa mawazo yao badala ya kuyazuia.


Pia ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake licha ya kuwa Rais wa nchini bado hakujali nafasi yake kwani aliamini katika utu na hivyo alikuwa anafikika kwa urahisi na akipenda kujikweza kwa cheo chake kwa kujiona yeye ni Bora au yuko juu zaidi ya Watanzania, siku zote alijishusha na kujiweka kundi la watu wa kawaida sana.


Kikwete ameyasema hayo leo Oktoba 8,mwaka 2019 wakati anafungua Kongamano lililoandaliwa na Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo katika kongamano hilo viongozi mbalimbali wastaafu na waliopo katika utumishi wamehudhuria .


Wakati Kukwete anazungumza katika kongamano hilo ametumia nafasi hiyo kuzungumza masuala mbalimbali yanayohusisha mchango wa Mwalimu Nyerere katika kujenga misingi imara ya Taifa letu ambapo amewataka Waatanzania kuendelea kuienzi na kusimamia kwa maslahi mapana ya nchi yetu.


"Mwalimu Nyerere aliamini kwenye utu,hivyo cheo chake cha Rais hakikusababisha ajione yeye ni Bora zaidi ha wengine,alijishusha na kila mtu alimfikia.Unapokaa na Mwalimu Mwalimu Nyerere unakuwa huna hofu .Ukiwa na cheo bado hakukuondolei ubinadamu wako, "amesema Rais mstaafu Kikwete.


Akizungumzia zaidi Mwalimu Nyerere, Rais huyo mstaafu amesema kuwa Mwalimu hakuwa na kinyongo na mtu eti kwasababu ametoa mawazo tofauti ya na kwake kwani eliminj katika Uhuru wa mawazo na mawazo hayapigwi rungu bali yanajibiwa kwa mawazo bora zaidi na hatimaye mambo yanakwenda vizuri.


"Hata CCM ni Chama nyenye maarifa mengi sana na kinachotumia akili lakini msingi wake mkubwa Mwalimu aliruhusu Uhuru wa mawazo.Niwakumbushe mwaka 1992 uamuzi wa busara kafanyika kwa kuingia katika mfumo wa vyama vingi,iliundwa tume wakati huo kukufanya maoni ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Jaji Fancis Nyarari.


"Wakati ule upepo wa vyama vingi ulikuwa unakuja.Ukafanyika utafiti kupitia tume hiyo ambapo asilimia 80 walitaka mfumo wa Chama kimoja na asilimia 20 Chama kimoja. Mimi nilikuwa wa Kamati Kuu,si haba nimekaa ...mjadala ulikuwa mkubwa na mkali, hata hivyo ikaamriwa asilimia 20 wameshinda na ilikuwa uamuzi wa kimkakati.


"Chama hiki kina maarifa mengi, na msingi mkubwa CCM wana uhuru wa mawazo.Kupoteza uhuru wa mawazo ndani ya Chama ni kwenda kukiharibu.Mwalimu alikuwa na akili sana ,yeye peke yake ni sawa na wajumbe 500.Alikuwa na uwezo wa kuchambua na anawasikiliza na kisha anakuja na samari yake ambayo inamaliza hoja zote ambazo hazikuwa na maana"amesema Kikwete.


Amesisitiza Mwalimu hakuna na kinyongo na mtu mwenye mawazo tofauti na yeye,alikuwa na moyo mzuri sana."Niwakumbushe wakati wa uhujumu uchumi tulikutana Karimjee na ajenda ikawa ajenda ya uhujumu uchumi.Kuna mjumbe mmoja alimwambia Mwalimu hawezi kuchukua zilizo ili akamwachia Sokoine kupambana na wahujumu uchumi , lakini Mwalimu alicheka tu.


'Wazee walitaka kumjua aliyeshauri vibaya...lakini aliwajibu washauri wake wa nini,kwani ni washauri wake,hivyo washughulike na yeye."Mwalimu anatufundisha kama  ulishauriwa ukakubali lawama zibaki za kwako na sio kumlaumu aliyekushauri.


Kikwete amesema kongamano ambalo limeandaliwa na Chuo hiko ni muhimu na la kupongeza kwani kinatoa fursa ya kukumbuka yale yaliyofanywa na Mwalimu na kuongeza Mwalimu kukumbukwa ni jambo ambalo anastahili, wala sio hisani na kwanini amefanya mambo mengi kwa Tanzania na Afrika na hata kwa duniani na utaamua kuyaorodhesha utakesha.


Ametaja baadhi ya mambo ambayo Mwalimu ameyafanya kwa ajili ya nchi ni kwamba Mwalimu ndio mkombozi wetu kwani ametukomboa kwa kututoa katika ukoloni.Mwalimu aliamua kuanzisha safari ya kuondoa ukoloni na ndipo Tanu ikaanza na Mwalimu akawa Rais, na baada ya uamuzi huo Serikali ya Mkoloni ikamtaka kuchagua abaki Tanu awe au Mwalim lakini yeye akaamua kubaki kuwa Mwalim.


"Ni uamuzi mgumu lakini kwa moyo wake wa upendo aliamua kujitoa yeye kwa ajili ya wengine. Hilo ni jambo kubwa sana kwa kuonesha moyo wa kujitolea, wangapi leo wanaweza kujitolea maana hata mshahara ukiwa mdogo watu wanaandamana.


"Mwalim Nyerere alikuwa na karama ya maneno na tumepata Uhuru kwa maneno, usione vyaelea ujue vimeundwa, umahiri wake ndio umetufikisha hapo. Kwa wenzetu imeshindikana hadi wanatumia nguvu. Tatu Mwalimu aliamini kwenye umoja na ndio maana kwa kushirikiana na swahiba wake mzee Karume walianzisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikuweo kwenye ramani ya dunia lakini hao wazee wameweza kuanzisha nchi yetu na mafanikio yake sote tunayaona.


Jambo la nne Mwalimu amesaidia kujenga taifa lenye umoja , amani na mshikamano, nchi yetu hii ina kabila zaidi ya 120 lakini wote tumebaki kuwa wamoja.Kulikuwa wamoja.Kulikuwa watu wenye dini na wasio na dini lakini tukabaki na umoja wetu,"amesema Kikwete na kuongeza tukianza kubaguana kwa dini au kabila hatutabaki salama.


Wakati jambo la tano la kukumbuka,Kikwete amesema Mwalimu alikuwa mtu wa kawaida mbele ya watu wengine.Ukikaa na Mwalimu hupati hofu ya kuwa naye kwani alikuwa ni Rais aliyejishusha na alikuwa wa kawaida.Alifanya hivyo kwa kuamini kuwa Rais haina maana wewe ni zaidi ya watu wengine.


"Ni jambo nzuri kutambua kujishusha na unapojishusha hakuondoi nafasi yako, ukiwa binadamu hakuondoi nafasi yako.Jambo la sita aliamini Uhuru wa Tanganyika hauna maana kama nchi nyingine za Afrika hazitakuwa zimejikomboa kutoka mikono ya wakoloni Mwalimu alifanya kila linalowezekana kukomboa nchi nyingine za Afrika,"amesema Kikwete kwenye kongamano hilo.


Alizungumzia pia Mwalimu Nyerere alivyokuwa anawapenda vijana na akakumbusha hata yeye(Kikwete) mwaka 1968 akiwa kidato cha tatu alikuwa kiongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana Kibaha na kwamba mwaka1982 akapata nafasi ya kuingia Halmashauri Kuu ya CCM.UVCCM ndio sehemu ya kujifunza fursa ya uongozi.Nimeingia Halmashauri Kuu ya Chama mwaka huo na hapo ukawa mwanzo na mwisho wa siku nikawa Rais.


'Kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu, niwapongeze Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuandaa kongamano hili.Baadhi ya mambo wamekuwa tunu ya taifa na lazima. hizo tunu tuzilinde.Kwa Tanzania hii sote ni wamoja pamoja na kuwa na makundi mbalimbali ya watu.


"Watanzania wenzangu, wanachama wenzangu tushikamane katika kusimamia tunu ya amani.Amani haina Chama ,dhehebu wala kabila.Umoja hauna chama,kabila wala dini.


Makongamano hayo ni muhimu kwani kukumbusha mambo ya msingi ya taifa letu,"amesema Kikwete.

Mgeni rasmi kwenye Kongamano la kuadhimisha miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa amesimama Meza kuu akiwa na viongozi wengine baada ya kumalizia kwa wimbo wa Taifa.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria Kongamano la Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere wakiwa ukumbini kabla ya kuanza kwa kongamano hilo ambalo limefanyika leo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akisaliamiana na baadhi ya wananchi waliohudhuria Kongamano la kumbukumbu ya kuadhimisha miaka 20 ya kifo ch Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.Kongamano hill ambalo  limeandaliwa  na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere limefanyika leo Oktoba  8,2019



No comments:

Post a Comment