Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua
Mwongozo wa uwekezaji Mkoani Pwani katika Kongamano la Uwekezaji
Mkoani Pwani alilolifungua kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo.
......................................
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka
mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo lake la kuandaa makongamano ya uwekezaji
ihakikishe inafanya hivyo mara moja.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumamosi, Oktoba 19, 2019) wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji kwa mkoa wa
Pwani katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza
viongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutekeleza agizo nililolitoa Juni 18, 2018 wakati
wa kongamano la tatu la uwezeshaji wananchi kiuchumi la kuhakikisha mikoa yote
inaandaa kongamano la uwekezaji na inakuwa na mwongozo wa uwekezaji wa mkoa.
Mikoa ambayo haijatekeleza agizo hilo, ifanye hivyo mara moja,” amesema.
Waziri Mkuu amesema mkoa huo umeweza
kubaini fursa zilizopo katika mkoa wa Pwani na kuzitangaza kupitia mwongozo wa
uwekezaji ambao pia ameuzindua leo.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo isemayo: ‘‘Ijenge Tanzania, wekeza Pwani mahali sahihi kwa uwekezaji
(Build Tanzania, Invest in Pwani, the Best Place for Investment)” ina maana
kuwa, licha ya mkoa wa Pwani kubainisha na kutangaza fursa za uwekezaji na
biashara zilizopo, unajipambanua vizuri na kuonyesha kuwa ni kwa namna gani
umejiandaa na umetengeneza mazingira bora yanayovutia wawekezaji wa ndani na
nje.
“Ili kudhihirisha dhamira ya dhati ya
kukuza uchumi kupitia viwanda, nimeelezwa kuwa mkoa umetenga hekta 53,016 kwa
ajili ya uwekezaji wa viwanda ambavyo vitatumia rasilmali zilizopo ndani ya
mkoa na maeneo mengine ya nchi kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na
kuboresha maisha ya wanachi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri
wahakikishe wanasimamia miundombinu inayoelekea kwenye viwanda vilivyopo kwenye
maeneo yao.
“Kila mmoja ahakikishe maji,
umeme na barabara vinafika kila eneo ambalo mwekezaji anataka kujenga
kiwanda. Nitumie fursa hii kuwaomba mlete mabadiliko chanya yanayotokana na
maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano.”
Mapema, akimkaribisha Waziri
Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji), Bibi Angella Kairuki alisema kwamba Serikali imeanza
kutekeleza mapendekezo ya mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji nchini (Blueprint for Improving Business Environment Regulatory
Licensing in Tanzania) kwa kuondoa tozo 163 zilizokuwa zikilalamikiwa na
wawekezaji.
“Pia tumetenganisha majukumu ya TBS
ya TFDA ambayo sasa ni TMDA. TBS itashughulika na vyakula na TMDA itashughulika
na dawa na vifaatiba. Vilevile, tumeondoa ada za usajili sehemu za kazi ambazo
zamani ilikuwa ni sh. 28,000 na sasa hivi zinatolewa bure,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi
Evarist Ndikillo aliwataka watu wote wanaotaka kuwekeza nchini waufikirie
kwanza mkoa wa Pwani kwa sasabu uko kimkakati na una fursa nyingi ikiwemo hali
nzuri ya usalama na kwa maana hiyo mitaji yao italindwa.
“Mkoa wetu uko kwenye eneo la
kimkakati la kuwezesha biashara kwa kuwa uko karibu na bandari ya Dar es Salaam
na uwanja wa ndege; uko karibu na soko kubwa ambalo ni Dar es Salaam; unapitiwa
na reli zote kwenda mikoani na nchi jirani; unapitiwa na barabara kuu itokayo
Dar es Salaam na pia una bandari kavu ya Kwala.”
Mbali ya hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa
alisema faida nyingine ambayo mkoa huo unayo ni uwepo wa miundombinu ya maji,
umeme na nishati ya gesi asilia ambayo imeanza kutumiwa na baadhi ya viwanda
kama Goodwill na Lodhia Steel.
Naye Dkt. Tausi Kida, Mkurugenzi wa
Taasisi ya Uchumi ya Kijamii (ESRF) ambayo ilisimamia uandaaji wa mwongozo wa
uwekezaji kwa mkoa wa Pwani, alisema taasisi yao inasaidia kuandaa na kuchambua
fursa zilizopo kwenye mikoa mbalimbali.
“Hadi sasa tumekwishaisadia mikoa 17
kuandaa miongozo ya uwekezaji na kwa sasa mikoa 12 imeshakamilisha na mikoa
mitano iko kwenye hatua mbalimbali,” alisema.
Akitoa taarifa kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela ambao ni wadhamini wakuu, Afisa
Mkuu wa Biashara, Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts alisema benki hiyo
imeendelea kugusa sekta zote za uchumi na hivyo kuongeza tija kwenye mnyororo
mzima wa uzalishaji.
Alisema huduma zao zimelenga kuongeza
tija na ufanisi katika sekta ya viwanda nchini ikiwemo utoaji wa mikopo ya
biashara kwa ajili ya kuongeza mikopo ya uendeshaji (working capita loans) na
mikopo ya uwekezaji (investment loans).
“Benki yetu inatoa mikopo ya biashara
na uwekezaji katika maeneo mbalimbali ambapo mikopo ya kilimo ni shilingi
bilioni 357, uzalishaji wa viwanda (shilingi bilioni 214), biashara (shilingi
bilioni 347), mahoteli (shilingi bilioni 87) na sekta ya madini (shilingi
bilioni 91),” alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza wakati alipofungua Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Pwani
kwenye ukumbi wa Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Pwani mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akionyesha Mwongozo wa uwekezaji Mkoani Pwani baada ya kuuzindua katika
Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Pwani alilolifungua kwenye ukumbi wa Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019. Kulia
ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki na
kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Uwekezaji
Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua
Kongamano hilo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani mjini
Kibaha, Oktoba 19, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Elibariki Parsalam kuhusu utengenezaji
wa chakula cha kuku wakati alipotembelea banda la kampuni ya Hill Feeds
katika Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Pwani alilolifungua kwenye ukumbi wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Oktoba 19, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkuu
wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo wakitazama malighafi ya Pazolana
inayotumika kutengeneza Saruji wakati Waziri Mkuu alipotembelea banda la
kampuni ya saruji ya Tanga katika Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa
Pwani lililofunguliwa na Waziri Mkuu kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Pwani mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019. Wa pili kushoto ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji), Angela Kairuki na kushoto ni Mtendaji
Mkuu wa kampuni hiyo, Mhandisi Benedict Lema.
No comments:
Post a Comment