Wednesday, October 16, 2019

SIMAMIENI FEDHA ZA SERIKALI,: WAITARA

Na Alodia Dominick, Bukoba.

Naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara amewataka viongozi kuanzia ngazi ya mkoa kwenda chini kusimamia fedha za serikali ambazo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kila chumba cha darasa ambazo ni shilingi milioni 12.5.

Naibu waziri Waitara ameyasema hayo leo akiwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera baada ya kufika mkoani hapa kwa ziara ya siku nne.

Amesema, katika kukamilisha chumba cha darasa ambacho jamii inakuwa tayari imeishaweka nguvu zake hadi usawa wa lita serikali inachangia milioni 12.5 kwa ajili ya vifaa vya viwandani ili kukamilisha ujenzi wa chumba hicho.

Waitara ameongeza kuwa, wazazi lazima washirikiane na serikali pale wanapotakiwa katika swala la elimu na kuwa viongozi kupitia bodi za shule wawambie wananchi kuwa michango inaruhusiwa kwani serikali haiwezi kufanya kila kitu.

"Katika kutoa elimu lazima tushirikiane wazazi na serikali na michango inaruhusiwa kwa utaratibu ambao uliwekwa na serikali ambao hauwahusishi walimu kupokea michango hiyo". Alisema Waitara.

Kwa upande wake Afisa elimu mkoa wa Kagera Juma Mhina ameeleza kwamba, serikali imetoa shilingi bilioni moja katika mkoa wa Kagera kwa ajili ya vyumba vya madarasa shule za msingi na shilingi bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari.

No comments:

Post a Comment