Friday, October 11, 2019

MSIPENDE KUPELEKANA MAHAKAMANI: WAKILI.

Wakili wa kujitegemea Jovin Rutainulwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
...............................


Na Alodia Dominick , Bukoba

Wananchi mkoani Kagera wameaswa kujiepusha na masuala ya kukimbilia mahakamani kushitakiana badala yake wamalize migogoro yao kwa kutumia wana familia, na viongozi wa dini katika kukwepa kupoteza muda wa kufanya shughuli za kimaendeleo katika jamii.

Ushauri huo umetolewa jana na Wakili wa kujitegemea Jovin Rutainulwa wakati akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake katika manispaa ya Bukoba mkoani humo ambapo ilikuwa siku ya kupinga adhabu ya hukumu ya kunyongwa duniani.


Wakili Rutainulwa amesema wananchi wanapaswa kuepukana na masuala ya kukimbizana mahakamani kwa migogoro midogo midogo ambayo inaweza kumalizwa na viongozi wa dini pamoja na wanafamilia badala yake watumie muda wa kwenda mahakamani kwa kufanya shughuli za kujiingizia kipato.


‘’Mahakama huzaja kesi ambazo nyingine hupaswa kuishia katika ngazi ya jamii na kesi nyingi hazina msingi ni za kupoteza gharama, muda na kujenga chuki zisizokwisha wananchi acheni kukimbilia mahakamani tafuteni njia mbadala za kutatua migogoro yenu labda Pale inaposhindikana ndo mahakama ihusike’’. Alisema wakili Jovin Rutainulwa.



Ametoa wito kwa mahakama kuendelea na mfumo walio nao wa kupunguza mashauri mahakamani kwa njia ya usuluhishi na kusikiliza kesi kwa haraka huku akitoa pongezi  kwa Wanasheria wa serikali na wa kujitegemea kwa kazi wanazofanya katika kuhakikisha wateja wao wanapata haki zao kwa muda na kwa mujibu wa sheria.

Cletus France mkazi wa Bukoba vijijini amesema, jamii ya mkoa wa Kagera inapaswa kubadilika kwa kubadili tabia ya kupenda kushitakiana mahakamani kwani jambo hilo licha ya kupoteza muda pia hupoteza rasilimali fedha na kurudisha maendeleo nyuma.
 

No comments:

Post a Comment