Thursday, October 3, 2019

BIDHAA ZA MAGENDO ZATEKETEZWA BAGAMOYO.

Afisa Mwandamizi wa Forodha Bagamoyo Noeli Makere akizungumza na waandishi wa habari.
..................................

Bidhaa zenye thamani ya Shilingi milioni 25, zimeteketezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kitengo cha forodha Wilaya ya Bagamoyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya yhiyo, kupitia Idara ya Afya, Usafi wa mazingira na Udhibiti wa taka ngumu pamoja na Jeshi la Polisi.


Uteketezaji huo umefanyika jana Oktoba 02, 2019 katika dampo la Sanzale lililopo Kata ya Magomeni baada ya kubainika kuwa zimeingizwa kwa njia za magendo, huku Serikali ikiwa imepiga marufuku bidhaa hizo kuingizwa Nchini kwani hazifai kwa matumizi ya binadamu na hazina ubora.


Bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na betri dazeni 12, Matairi ya magari na pikipiki yaliyotumika (Used Tyres) 400, Nguo za mitumba balo 9, vilainishi ‘lubricants’ lita 960, mafuta ya taa lita 300, Friji 2, kompresa za friji 12 na sabuni za unga Kilo 30 vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya jumla ya Shilingi Mil. 25,949,001/-


Afisa Mwandamizi wa Forodha Bagamoyo Noel Makere akizungumza wakati wa uteketezaji huo amesema bidhaa hizo ni za magendo na zilikamatwa katika doria zinayofanywa na Ofisi ya Forodha.


“Matairi haya 400 tunayoteketeza yamekatazwa kabisa kuingizwa na kutumika Nchini, huku bidhaa kama friji na mitumba ni bidhaa zilizozuiwa kuingizwa Nchini, Alisema Makere.


Bidhaa za betri, mafuta ya taa na vilainishi ni bidhaa tunazoteketeza kutokana na kukosa ubora wakati zinakamatwa. Aliongeza Makere.
  

Alibainisha kuwa, bidhaa zote hizo zilizoteketezwa  zimethibishwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.



Aidha, alitoa onyo kwa Wafanyabishara kuwa wazalendo na kufuata sheria na taratibu za uingizaji bidhaa Nchini hususani ulipaji wa kodi ili kuepuka usumbufu na hasara zisizo za lazima.


Alisema idara ya forodha imekuwa ikitoa elimu na huduma bure kwa wafanya biashara ili kuwasaidia kufanya biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu za Nchi.


Alimalizia  kwa kusema kuwa, idara ya forodha wilaya ya Bagamoyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wamejipanga kuhakikisha bidhaa zote za magendo zinazotishwa Bagamoyo zinadhibitiwa ili kodi ya Serikali isipotee”.


Naye Afisa Afya wa Wilaya ya Bagamoyo Bw. Mohamed Farah aliyesimamia uteketezaji wa bidhaa hizo, amewasihi wafanya biashara kutii sheria bila shuruti na kuhakikisha bidhaa wanazoingiza Nchini kupitia Bandari ya Bagamoyo, hazina madhara kwa watumiaji ili kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zilizokosa ubora na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu
Image may contain: fire and outdoorImage may contain: cloud, sky, mountain, fire, outdoor and nature
Picha ni bidhaa hizo zikiteketezwa katika eneo la Sanzale

No comments:

Post a Comment