Monday, November 5, 2018

PWANI YATILIANA SAINI MKATABA WA USAMBAZAJI DAWA ,VIFAA TIBA KUPITIA MSHITIRI MMOJA

Katibu tawala wa mkoa wa Pwani Theresia Mbando (wa pili kulia ) na mkurugenzi wa Astra Pharmacy Ranjiy Jha(wa kwanza kushoto ) wakitia saini mkataba wa usambazaji wa dawa ,vifaa tiba na vitendanishi kwa kupitia mfumo wa mshitiri mmoja (prime vendor system),wa kwanza kulia ni mfamasia wa mkoa Elias Mabonesho
.....................................

NA MWAMVUA MWINYI,PWANI

MKOA wa Pwani,umefikia asilimia 90 ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ,hadi kufikia octoba 2018, hatua ambayo inaelekea kwenda kupunguza kero ya upungufu wa dawa na vifaa hivyo kwenye vituo vya afya.

Hayo yalibainika ,wakati wa kikao cha mkoa cha zoezi la kusaini mkataba wa usambazaji wa dawa ,vifaa tiba na vitendanishi kupitia mfumo wa mshitiri mmoja (prime vendor system),zoezi ambalo limefanywa baina ya katibu tawala wa mkoa Theresia Mbando na mkurugenzi wa Astra Pharmacy Ranjiy Jha.

“Kwa mujibu wa taarifa zinavyotolewa katika mfumo wa kukusanya na kuchambua data za afya (DHIS 2 ),hadi kufikia kipindi hicho wamefikia asilimia hiyo jambo ambalo limenifurahisha” alisema Theresia .

Theresia alisema ,kwa hatua waliyofikia mzabuni huyo anatarajiwa atafikisha lengo la upatikanaji wa dawa kwenye vituo na halmashauri za mkoa kwa asilimia 100.

“Wananchi wamekuwa wakilalamikia juu ya upungufu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyetu hivyo ni imani yangu kwa hatua hii ,itakuwa muarobaini wa malalamiko hayo “

Aidha alisema,  kumekuwa na wastani wa utimilizaji wa oda kwa kiwango ambacho ni cha kubadilika badilika kutoka bohari ya madawa (MSD).

“Kufuatia uwepo wa mshitiri huyu naamini kwa bidhaa ambazo hazijatimia utimilifu kama ziliombwa bohari ya madawa zitajaziwa na mshitiri na hilo ndilo lengo kuu “alifafanua Theresia .

Kwa mujibu wa Theresia, baada ya kusaini mkataba huo halmashauri hazitakiwi kutumia wazabuni wengine na badala yake zitatakiwa kununua kwa mzabuni aliyepatikana kisheria kupitia mchakato uliofanywa na OR-TAMISEMI mwaka 2017.

Nae mfamasia wa mkoa wa Pwani Elias Mabonesho ,alielezea mfumo huo ulianzia Dodoma kama majaribio na kwasasa uko katika mikoa ya Morogoro ,Shinyanga na sasa Pwani .

Anasema ,mfumo utasimamiwa na ofisi ya katibu tawala wa mkoa kupitia ofisi ya uratibu wa mfumo wa mshitiri mmoja chini ya Mganga mkuu wa mkoa akisaidiwa na mfamasia ambae ndie mratibu huu .

Kwa upande wa wakurugenzi na waganga wakuu wa wilaya ,akiwemo mkurugenzi wa Mafia ,Erick Mapunda alisema ,kwa mfumo wa Jazia tatizo la ukosefu wa dawa linakwenda kuwa historia

No comments:

Post a Comment