DAWA za kulevya ni moja kati ya
vitu vyenye madhara makubwa ambavyo vinachangia kuporomosha uchumi wa Taifa kwa
sababu yanaathiri vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi.
Hata hivyo dawa za kulevya
zimekua zikiigharimu Serikali kwa kutumia fedha nyingi katika kupambana na
athari zitokanazo na matumizi dawa hizo, hivyo imewataka wananchi na jamii
kiujumla kutojihusisha na biashara hiyo haramu.
Mbali na dawa hizo kulisababishia
Taifa madhara ya kiuchumi na kiafya, pia biashara hiyo ya dawa za kulevya
inachafua na kushusha hadhi ya Tanzania kimataifa.
Madhara ya kiafya
yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika kwa
mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwa ni pamoja na kuchanganyikiwa, kuwa na
ulevi uliopindukia na hatimaye kusababisha kifo kama mtumiaji atazidisha
matumizi.
Katika kuhakikisha biashara hiyo
inakomeshwa Serikali imeunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya
nchini ambayo ndiyo inayoongoza mapambano hayo.
Jumatano ya Machi 22, mwaka huu
akiwa nchini Mauritius, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na Watanzania
waishio nchini huko katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya Meridien mjini
Port Louis.
Akizungumza na Watanzania hao
aliwataka wajiepushe na masuala yahusuyo dawa za kulevya. Aliwataka Watanzania
wote wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika na kamwe
wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Vita ya dawa za kulevya ni
kubwa, hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza
vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya.
Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” alisema.
Alisema katika kudhibiti biashara
hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na tutakamata
kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo, uwezo na mamlaka
aliyonayo,”.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo
inafanya kazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo
likiwa ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na
madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.
Waziri Mkuu alisema kuna
Watanzania wengi wamefungwa katika magereza mbalimbali duniani na wengine
wamehukumiwa kunyongwa baada ya kuthibitika kuwa wanajihusisha na
matumizi, usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, hivyo aliwataka wawe
mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kujiepusha na dawa za kulevya.
Akizungumzia idadi ya watu ambao
hadi sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali, Waziri Mkuu alisema takwimu
za jumla zinaonyesha kuwa Watanzania 515 wamekamatwa na kufungwa gerezani kwa
makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa ya kulevya.
“Nchini China Watanzania walioko
magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran wako Watanzania
63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako Watanzania 296,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba
“Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Vita hii
inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa
za kulevya ni kubwa. Sote kwa pamoja tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo,”
alisisitiza.
Kwa mujibu wa taarifa
zililizopatikana ndani ya Jeshi la Magereza Tanzania hadi Machi 26, mwaka huu
kulikuwa na wafungwa 512 wanaotumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali
kutokana na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, ambapo kati yake wanaume
ni 491 na wanawake 21.
Mbali na wafungwa pia kuna
mahabusu 1,284 wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na utumiaji,
usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, ambapo kati yao wanaume ni1,166 na
wanawake ni 118.
Katika hatua nyinngine, Waziri
Mkuu aliwataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa
pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa kutangaza
vivutio vya Taifa.
Alisema ni vema wakatumia fursa
walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na kuwekeza
kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha
na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed
aliwaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa umoja wao
ndiyo nguzo yao.
“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta
elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha
maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie kilichowaleta,”
amesema.
Dkt. Khalid aliwahakikishia
Wanzania hao walioko nje ya nchi kuwa Tanzania iko salama na wanaendelea
kudumisha amani na utulivu kama walivyoiacha wakati walipondoka.
Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja
wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni Ofisa wa
benki ya Standard Chartered nchini Mauritius alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba
kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza Tanzania kwa lengo la kukuza
uchumi wa Taifa.
Alisema wanaunga mkono na
kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika
kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi wa
miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha uwajibikaji na
nidhamu kwa watumishi wa umma.
Bw. Kongwa alisema Tanzania ina
nafasi kubwa ya kujifunza mambo mbalimbali nchini Mauritius kama namna bora ya
kuendesha kilimo cha miwa kwa sababu nchi hiyo inazalisha zaidi ya tani 600,000
za sukari kwa mwaka na tani 530,000 inauzwa nje ya nchi.”Tutumie fursa hii
kujifunza zaidi ili tuweze kukuza uchumi wetu,”.
Aliongeza kuwa mbali na kujifunza
kilimo cha miwa pia Tanzania inaweza kutangaza vivutio vyake vya utalii nchini
Mauritius ili kuwawezesha watalii wengi wanaoingia nchini humo kuweza
kuvifahamu na hatimaye kuwa nchini. Kwa mwaka Mauritius inapata watalii zaidi
ya milioni moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
IJUMAA, MACHI 31, 2017.
No comments:
Post a Comment