Sunday, November 4, 2018

KALEMANI:ILI KUONDOA ADHA YA KUKATIKA UMEME

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akikagua miundombinu ya kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mwakibete, Jijini Mbeya na kuagiza mafundi na wahandisi katika Vituo vyote nchini kufanya ukaguzi wa kila siku kuepusha kukatika Umeme kutokana na hitilafu zinazojitokeza katika Vituo hivyo.
 

Mameneja wote wanaosimamia vituo vya kupoza na kusambaza umeme nchini wametakiwa kufanya ukaguzi ( checkup) wa kila siku asubuhi katika mitambo na mashine zilizopo katika vituo hivyo kuondoa adha ya kukatika umeme kutokana na hitilafu au uharibifu katika vituo hivyo.

Licha ya kuwa vituo hivyo vinafanyiwa ukarabati na ukaguzi wa kila mara au hata baada ya miezi kulingana na utaratibu waliojiwekea.
Hayo yameleezwa na Waziri wa Nishati ,Dkt. Medard Kalemani , wakati wa ziara yake ya kikazi katika Jiji la Mbeya, Novemba 3, 2018, baada ya kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo Mwakibete na kukagua miradi ya kusambaza umeme katika kijiji cha Nsalaga na Iduda inayotekelezwa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).

Alieleza kuwa kumekuwa na changamoto ya kukatika umeme kwa muda mchache katika baadhi ya maeneo na sababu kuu ya ikielezwa kuwa ni hitilafu katika vituo au kuharibika kwa kifaa katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme.

Alifafanua kuwa changamoto hiyo inaepukika na kutoweka kabisa endapo wahandisi na mafundi watakuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa mitambo na mashine zao kila siku asubuhi kubaini tatizo kabla ya kutokea.

Mafundi na wahandisi muwe na tabia ya kufanya ukaguzi na matengenezo ya kila siku asubuhi badala ya kusubiri tatizo litokee, acheni kufanya ukaguzi na matengenezo kwa mazoea, hii itasaidia kufahamu mapema tatizo linazoweza kutokea baadaye na kuondoa usumbufu wa kukatika umeme kwa wananchi hali ya kuwa kuna umeme mwingi nawa kutosha, alisisitiza Kalemani.

Alifafanua kuwa kwa sasa serikali haitaki kuona mtu yeyote anakosa huduma ya umeme kwa muda Fulani kwa sababu tu kumetokea ya hitilafu katika mitambo na mashine katika vituo vya kupoza na kusambaza umeme, badala yake inataka umeme upatikane saa 24 na siku saba kwa wiki kwa kuwa umeme upo wa kutosha na ziada.

Waziri wa Nishati, Dk.Medard Kalemani, (katikati) akipita katika mitaa ya kijiji cha Nsalaga kukagua Miundombinu ya usambazaji wa huduma ya Umeme, unaotekelezwa na Shirika la Umeme,  nchini (Tanesco) ambapo ametoa siku 14,kwa wananchi hao kuunganishwa na huduma hiyo.


No comments:

Post a Comment