Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na
Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nishati wa
Misri Dkt. Mohamed Shaker, Waziri wa Nishati Medard Kalemani pamoja na viongozi
wengine akisikiliza namna mradi wa Kuzalisha umeme Megawati 2115 katika eneo la
mto Rufiji utakavyokuwa ukifanya kazi mara baada ya kukamilika.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na wananchi kabla ya kuweka jiwe la msingi mradi wa Kuzalisha umeme Megawati
2115 katika eneo la mto Rufiji.
.................................
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli leo tarehe 26 Julai, 2019 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa
mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji Mkoani Pwani ambao utakamilika Juni
2022 na kuzalisha megawati 2,115.
Sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo
zimefanyika kando ya eneo litakapojengwa bwawa la maji na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson,
Waziri wa Nishati wa Misri Mhe. Dkt. Mohamed Shaker, Mawaziri na Naibu Mawaziri
wa Tanzania, Wabunge, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa
Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na
viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Ujenzi wa mradi huo utagharimu shilingi za Kitanzania
Trilioni 6.5 na bwawa litakalojengwa litakuwa la kwanza kwa ukubwa Afrika
Mashariki na la nne kwa ukubwa Barani Afrika, na Mhe. Rais Magufuli
amependekeza bwana hilo liitwe Bwawa la Nyerere ikiwa ni kutambua na kuenzi
maono ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyetaka kujenga
bwawa hilo wakati wa uongozi wake.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya
Nishati kwa kusimamia utekelezaji mradi huo na ameeleza kuwa Serikali imechukua
hatua za kujenga bwawa hilo ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kutoka
megawati 1,601 zinazozalishwa hivi sasa, hadi kufikia megawati 10,000 ifikapo
mwaka 2025.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kutekeleza mradi huo,
Serikali itajenga mradi wa kuzalisha umeme katika mto Ruhudji utakaozalisha
megawati 359, mradi wa Lumakali megawati 222, mradi wa kakono megawati 87,
Rusumo megawati 80 na mingine itakayotumia nishati ya gesi, makaa ya mawe, jua,
jotoardhi, upepo na urani.
Amewataka wakandarasi wanaojenga mradi (Arab Contractors na
Elsewedy Electric za Misri) kukamilisha mradi huo kabla ya Juni 2022 hasa
ikizingatiwa hakuna tatizo la fedha ili Watanzania waanze kunufaika mapema.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Medard Kalemani amesema tayari
wakandarasi wanaojenga mradi huo wamelipwa asilimia 15 ya fedha zote za mradi
huo ambayo ni sawa na shilingi Trilioni 1.007 na kwamba ujenzi utahusisha bwawa
la maji lenye uwezo wa kukusanya mita za ujazo Bilioni 33.2, Jengo la mitambo
ya kuzalisha umeme litakalokuwa na mitambo 9, kituo cha umeme na njia ya
kusafirishia umeme yenye urefu wa kilometa 135 hadi kufika Chalinze.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema Wabunge wanampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
utekelezaji wa mradi huo na wanaamini kuwa umeme utakaozalishwa utawasaidia
Watanzania na pia kufanikisha miradi mikubwa inayotekelezwa katika awamu hii
ikiwemo ujenzi wa reli na ujenzi wa viwanda.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa amesema kuanza kwa ujenzi wa mradi huo ni mafanikio makubwa
ya Mhe. Rais Magufuli ambaye amedhamiria kuhakikisha kila nyumba ya Mtanzania
inapatiwa umeme.
Waziri wa Nishati wa Misri amewasilisha salamu za Rais wa
Misri, Mhe. Abdel Fattah El- Sisi ambaye ameahidi kufuatilia ujenzi wa mradi
huo unaofanywa na kampuni za Misri na pia ameahidi kuwa nchi hiyo itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa udhamini wa
masomo ya nishati jadidifu kwa wanafunzi 50 ambao watasaidia juhudi za kuongeza
uzalishaji wa umeme hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kujivunia
mafanikio haya makubwa ya kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na kutoyumbishwa
na wanaopinga utekelezaji wa mradi huo kwa kigezo cha uharibifu wa mazingira
kwani mradi huo utasaidia zaidi kutunza mazingira kwa watu kutumia umeme badala
ya kuni na mkaa zinazotokana na ukataji wa miti, na pia utasaidia kuwepo uvuvi,
kilimo cha umwagiliaji na kuinua utalii kutokana na Wanyama wengi kupata maji
ya uhakika.
“Kwenye
hili pori la Selous kuna hoteli za kitalii za gharama kubwa, kuna vitalu vya
utalii 47 na kuna uwindaji unaendelea, sasa haiwezekani sisi tukitaka kujenga
bwawa la kuzalisha umeme tuambiwe tunaharibu mazingira wakati eneo tunalotumia
ni chini ya asilimia 3 ya pori la Selous.
Mradi huu
umekumbana na upinzani mkali wa ndani na nje ya nchi, lakini kwa kuwa sisi ni
Taifa huru na sio masikini kama watu wanavyodhani, tumeamua kutekeleza mradi
huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza kumegwa kwa sehemu ya Pori la
Akiba la Selous ili iwe Hifadhi ya Taifa na amependekeza iitwe Hifadhi ya
Nyerere na sehemu yenye vitalu vya uwindaji iendelee, lengo likiwa kuimarisha
zaidi uhifadhi wa maliasili katika eneo hilo na kupata manufaa zaidi.
Ameagiza barabara ya kuunganisha eneo la mradi huo mpaka
Fuga ianze kujengwa kwa kiwango cha lami hatua kwa hatua ili kurahisisha
mawasiliano ya eneo hilo.
Pamoja na kutaka wananchi wa Morogoro na Pwani wapewe
kipaumbele katika ajira wakati wa mradi huo, Mhe. Rais Magufuli ameagiza mradi
huo kukatiwa bima ya Taifa, utoaji wa vibali vya kazi kwa wafanyakazi wa kutoka
nje ya nchi ufanyike haraka na vyombo vya ulinzi na usalama vya Morogoro na
Pwani vishirikiane kuulinda.
Pia amewataka viongozi na wananchi wa Mikoa yote yenye
vyanzo vya maji vinavyomwaga maji yake katika mto Rufiji kuhakikisha
wanavitunza vyanzo hivyo ili viendelee kuchangia maji mengi katika mto Rufiji.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Rufiji
26 Julai, 2019
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia
pamoja na viongozi wengine mara baada ya tukio hilo la uwekaji wa Jiwe la
Msingi.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza
Waziri wa Nishati wa Misri Dkt. Mohamed Shaker mara baada ya kuweka Jiwe la
Msingi mradi wa Ujenzi wa Kuzalisha umeme Megawati 2115 katika eneo la mto
Rufiji katikati ya Morogoro na Pwani.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia
michoro ya ujenzi huo mkubwa wa kufua umeme.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na Waziri wa Nishati wa Misri Dkt. Mohamed Shaker wakati wakielekea kwenda
kuweka jiwe hilo la msingi.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikata
utepe kuashiria uzinduzi wa mitambo itakayotumika katika mradi huo mkubwa wa
kufua umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia eneo la bonde katika mto Rufiji mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa umeme.
Eneo la
mto Rufiji ambalo litatumika katika ujenzi huo wa kufua umeme kama
linavyoonekana.
PICHA NA IKULU.
No comments:
Post a Comment