Thursday, July 25, 2019

WANANCHI BAGAMOYO WAPEWA ELIMU YA SHERIA.

Baadhi ya wanachi wa Bagamoyo wakiwa katika mahakama ya wilaya Bagamoyo ambao licha ya kufika kusikiliza kesi zao lakini pia walipatiwa elimu ya sheria kutoka kwa maafisa wa ustawi wa jamii.

...............................

Idara ya ustawi wa jamii wilaya ya Bagamoyo imeanzisha utaratibu wa kutoa elimu kwa uma ili kuelimisha jamii kuhusu sheria za makosa mbalimbali.


Akizungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG mara baada ya kumaliza kutoa elimu hiyo, Afisa ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya Bagamoyo anaehudumu katika mahakama ya wilaya Bagamoyo, Bi Flora Warioba amesema wanafanya hivyo ili kuwajengea uwezo wananchi wa kawaida katika kuzifahamu sheria.


Alisema elimu hiyo inawasaidia wananchi kujua haki zao za msingi na kipi cha kufanya ili kukabiliana na changamoto wanazozipata.


Aliongeza kuwa, elimu hiyo inayotolewa inaisadia jamii ya wananchi wa kawaida na kwamba kwa elimu hiyo pia hatimae wataweza kuelimishan wenyewe.


Alisema jamii ikielewa sheria itasaidia kupunguza migogoro inayotokea hasa katika maswala ya watoto kunyanyaswa, ubakaji, ulawiti na mengineo.


Aliongeza kuwa watu wengi hawajui hata akikamatwa na polisi kipi anatakiwa kufanya na hatua zipi za kufuata ili apate dhamana.


Kwa upande wao wananchi waliopata elimu hiyo walisema elimu iliyotolewa ni nzuri lakini haipo kwenye uhalisia katika ukitekeleza.


Walisema wananchi wengi wanaogopa vyombo vya ulinzi na usalama hali inayopelekea kushindwa kujitetea na hasa wanapokutana na vitisho vya aina mbalimbali kutoka kwa maaskari.


Dedan Masau ni mmoja wa watu waliopata elimu hiyo, alisema kutojua sheria miongoni mwa wananchi kunapelekea hata wanapoombwa rushwa inakuwa rahisi kutoa kwa kudhani kuwa rushwa inaweza kumuokoa na matatizo aliyo nayo au kupata haki yake.


"Sheria inamtia hatiani mtoa rushwa na mpokea rushwa hivyo wananchi wanapaswa kufahamu kuwa wanapoombwa rushwa wakitoa na wao wameingia kwenye makosa, Alisema Dedan Masau.


Miongoni mwa mambo waliyolalamikia washiriki hao ni pamoja na kupewa kesi ambazo sio zao na jeshi la polisi hali inayopelekea uzito wa kujitetea ili kujikwamua na kosa.


Hata hivyo upande wa polisi ulieleza kuwa, hakuna sheria ya kumpa mtuhumiwa kosa ambalo hakulifanya na kwamba kila kosa atakalopewa ni kutokana na tukio lililotokea.


Aidha, wananchi wameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuzingatia sheria ili kila mmoja apate haki yake anayostahiki bila upendeleo wa kumuonea mwingine.
 
Afisa ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya Bagamoyo anaehudumu katika mahakama ya wilaya Bagamoyo, Bi Flora Warioba akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa uma mahakamani hapo.



Afisa ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya Bagamoyo anaehudumu katika mahakama ya wilaya Bagamoyo, Bi Flora Warioba akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa uma mahakamani hapo.

Wanachi wakipata elimu ya sheria katika mahakama ya wilaya ya Bagamoyo.
  
Wanachi wakipata elimu ya sheria katika mahakama ya wilaya ya Bagamoyo.



No comments:

Post a Comment