Saturday, July 6, 2019

Wadau PS3, GHSC TA – TZ, Waunga Mkono Juhudi za Serikali ya Awamu ya tano





Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula akiongoza kikao cha pamoja baina ya Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Afya kilicho wakutanisha Wadau wa Maendeleo kujadili uboreshaji wa Mfumo wa GoTHOMIS ili uweze kutumika katika ngazi zote za kutolea huduma za Afya nchini (Picha na Maktaba ya TAMISEMI) 
…………………… 


Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA,Ofisi ya Rais TAMISEMI, Erick Kitali, akitoa mada wakati wa kikao hicho cha wadau juu ya uboreshaji wa Mfumo wa GoTHOMIS Ofisi za Wizara za Afya eneo la Mtumba mjini Dodoma. (Picha na Maktaba ya OR-TAMISEMI).

Na Atley Kuni- TAMISEMI. 

Wadau wa Maendeleo nchini kupitia mradi wa Uimarishaji Mifumo katika Sekta za Umma (Public Sector Strengthening System-PS3) na (Global Supply Chain Technical Assistance Tanzania-GHSC TA – TZ), wameitikia wito wa serikali na kujitokeza katika kufanikisha zoezi la kuimarisha mfumo wa Uendeshaji wa Shughuli za Afya katika maeneo yote yakutolea huduma za Afya serikalini, ujulikanao (Government of Tanzania Health Operations Management Information System -GoTHOMIS). Wadau hao wameitika wito kufutia maelekezo ya Serikali kutaka mfumo huo uimarishwe kwa kuongezewa maeneo ya kiutendaji. 

Akizungumza na Wadau wa Maendeleo mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2019 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula, wakati wa kikao cha pamoja baina ya Wizara hiyo na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) alisema, umefika muda kwa wadau kuungana na kujenga mfumo wa GoTHOMIS kwani mfumo huo umeonesha kuwa na tija na ufanisi kwenye nyanja ya Afya. 

“Kwa Muda mrefu tumeshuhudia mifumo mbali mbali lakini yote hii ikiwa kwenye maeneo machache ya nchi ikifanywa kwa majaribio ambayo hata hivyo tija yake imekuwa sio yakuridhisha, alisema Chaula na kuongeza kuwa, suala lakutuambia unafanya shughuli ya Jamii halafu hatuoni tija ya unacho kifanya sio wakati wake kwa sasa, lazima wote tuungane na tukubali kutembea kwa pamoja na mfumo huu ambao umeonesha tija na ufanisi” alisema Dkt. Chaula. 

Wito wa Katibu Mkuu huyo, ulikuja wakati ambapo tayari mfumo ulikuwa umesimikwa kwenye maeneo yakutolea huduma za afya yapatayo 383 ikiwepo Zahanati 91, Vituo vya Afya 180, Hospitali Teule za Wilaya 12, Hospitali za Wilaya 77 na Hospitali za Rufaa za Mikoa 23 na kufanya asilimia 6 ya maeneo yote yakutolea huduma za afya nchini. 

Akiwasilisha mada katika kikao hicho juu ya uboreshaji wa mfumo wa GoTHOMIS, Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Rais TAMISEMI, Erick Kitali, alisema shabaha iliyo mbele yao nikuimarisha mfumo kwa kutumia wataalam wazawa na wanaamini katika nguvu ya pamoja ikiwepo kushirikiana na wadau wa maendeleo wote. 


Akizungumza kando ya wataalam wanao endelea na kazi ya uimarishaji wa mfumo huo mkoani Morogoro, Mtaalam kutoka Global Supply Chain Tanzania, Alfredy Mchau, alisema wamewiwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha mfumo huo wa GoTHOMIS kwani ni moja ya vipaumbele vyao katika kushirikiana na serikali kuboresha huduma za Afya kwaajili ya upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati. 

“Alipotoa wito Katibu Mkuu, kwa wadau juu ya kuunga mkono suala hili, sisi kama Global Supply Chain Technical Assistance Tanzania (GHSC TA – TZ), tulielewa nini dhamira ya Serikali hii ya awamu ya tano inayo ongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, katika sekta ya Afya, ambayo kimsingi ndio msingi wa maendeleo ya nchi yoyote. 

Mchau aliongeza kuwa, GHSC TA – TZ ilikwisha anza harakati za uboreshai wa mfumo wa GoTHOMIS ili uweze kubadilishana taarifa na mfumo wa eLMIS ili kuboresha upatikanaji wa taarifa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchi nzima hivyo tunaamini kwa nguvu hii ya pamoja tutapiga hatua kubwa katika kuihudumia jamii, kwani Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu” alisisitiza Mchau. 

Kwa upande wake mmoja wa wafanyakazi kutoka mradi wa kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma nchini PS3 Mhandisi, Revocutus Mtesigwa, alisema huo ni muendelezo wa juhudi ambazo wamekuwa nazo hususan katika uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma nchini. 

“PS.3 Hii kwetu ni muendelezo wa shughuli ambayo tayari tulisha anza hapo awali, kwani tayari kuna maeneo yakutolea huduma za Afya yasiyo pungua 400 ikiwepo Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati tumewezesha kufungwa kwa mfumo na unafanyakazi, maeneo ambayo kama mradi tuliokwisha fanyia kazi ni eneo la Mafunzo kwa watumiaji, ufungaji Miundombinu ya Mtandao Kiambo (Local Area Network-LAN), hivyo Kauli ya Katibu Mkuu kwetu ilituongezea chachu na ari yakuendelea kushirikiana zaidi na Serikali lakini pia Wadau wengine wa Maendeleo katika kujenga nchi. 

Serikali bado inaendelea kuwakaribisha wadau wa maendeleo kujitokeza kwaajili yakufanikisha uboreshaji wa Mfumo wa GoTHOMIS, ambao utakuwa Madhubuti na wenye tija katika ngazi zote za kutolea huduma za Afya nchini.

No comments:

Post a Comment