Tuesday, July 2, 2019

VIJIJI 10,278 KUFIKIWA NA UMEME

Image may contain: Subira Mgalu, smiling, standing and closeup
Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imeeleza kuwa, Shirika la Umeme nchini Tanesco mpaka Juni mwaka 2020, vijiji vipatavyo elfu 10,278 vitakuwa vimeshaunganishiwa na huduma ya umeme.

 
Aidha kwenye zoezi hilo la uunganishwaji wa huduma hiyo, katika mpango uliowekwa na serikali unataraji kwamba mpaka ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote vilivyobakia 1,990 vitakuwa vimefikiwa na huduma hiyo.


Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza na wakazi wa Kitongoji cha Fitina Haina Posho, Kijiji cha Fukayosi wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo alisema kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa maeneo yaliyopitiwa na umeme mkubwa.


"Usambazaji wa miundombinu ya umeme ina gharama kubwa sana, kilometa moja inagharimu kiasi cha shilingi milioni 50, mpaka kuufikisha hapa sekondari yetu ya Fukayosi mradi huu umegharimu zaidi ya milioni miamoja," alisema Mgalu.


Ameongeza kwamba mwanzoni umeme ulivyofika katika maeneo ya Mwavi, Mkenge, Kidomole na sehemu nyingine, ilitakiwa REA iikabidhi mradi huo Tanesco ili kazi iendelee kwa kuanzia shilingi 170,000, 300,000 mpaka 500,000 kulingana na uhitaji wa nguzo.


Mgalu ametanabaisha kwamba, Tanesco haikuwa na ukiritimba wa kusambaza umeme, isipokuwa changamoto iliyokuwepo wakati huo ni uwezo wa kumudu gharama za uunganishaji wa huduma kwa wananchi.


"Mwaka huu wa fedha 2019/2020 Tanesco wameweka kipaumbele cha kuzalisha umeme wa ziada megawati 300 ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo tulikuwa na mapungufu ya megawati 100 kwa siku," alisema Mgalu.


Ally Ally Mwenyekiti wa halmashauri ya Bagamoyo ambae pia ni Diwani wa kata ya Fukayosi, alielezea changamoto zilizokuwepo awali shuleni hapo, zikiwemo umeme, barabara na maji, ambapo CHALIWASA waliweza kupeleka maji, pamoja na wadau wengine wakiwemo taasisi ya Goodneighbour pamoja na halmashauri.


Meneja wa Tanesco wilayani Bagamoyo Kidada Maeda alisema kuwa maeneo mengi hayajafikiwa na umeme na kwamba ofisi yake imelichukua hilo na wataliingiza katika mpango wa ujazilizi, pia wataiingiza katika REA awamu ya 3 sehemu ya 2.


Nae Mwenyekiti wa Kamati ya shule Josefa Lyimo ameshukuru taasisi ya Goodneighbour kwa msaada mkubwa unaopatikana shuleni hapo, huku akiomba umeme usambazwe kukabiliana na changamoto ya wizi, sanjali na kulilia hostel shuleni.

No comments:

Post a Comment