Anna Potinus
Rais Dk. John Magufuli ameonekana kumpigia ‘kampeni’ Mbunge wa jimbo la Kongwa, Job Ndugai baada ya kusema kuwa Mbunge huyo anatosha kuliongoza jimbo hilo na kwamba haina haja ya kumchagua kiongozi mwingine kwani mbunge huyo anaisaidia nchi nzima kwa nafasi yake aliyo nayo.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 18, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, ambapo amewataka wagombea waliogombea nafasi ya ubunge 2015, kuachana na mawazo ya kutaka kugombea tena kwani nafasi hiyo ni ya Ndugai.
“Ninawashukuru kwa kumchagua Mbunge wenu Ndugai, maana wakati mwingine ni vigumu kwa mtu wa pale pale watu wakajua huyu ni mfalme ndiyo maana katika maandiko wafalme wengi walikataliwa maeneo walipozaliwa lakini ninawambia kuwa mmechagua mtu ambaye anasaidia nchi nzima kwa nafasi yake na msingemchagua kuwa mbunge kwa vyovyote asingekuwa spika,” amesema.
“Ninafahamu wakati wa kampeni kulikuwa na wengine waliohitaji ubunge na nilipofika hapa niliwaambia kazi si ubunge na ukweli ni kwamba wale wote waliogombea niliwateua nafasi mbalimbali wengine wakawa wakurugenzi na wengine wakuu wa mikoa hivyo nitashangaa sana kama 2020 watakuja tena kugombea hapa na wakija wajue hizo nafasi zilizowapa hawataziona tena labda wajitokeze wengine,” amesema.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa muda umefika wa kulienzi Jimbo la Kongwa kutokana kubeba historia ya Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika
“Unapotamka Kongwa kwenye nchi ambazo zimepata uhuru kutokana na kujitolea kwenu wanaelewa, wapo walioacha hata damu zao hapa na wengine walizikwa hapa, baba wa taifa alipoamua kuzikomboa nchi zote za kusini mwa Afrika alitumia Kongwa kwa hiyo hapa kuna historia ya ukombozi.
“Ninakubaliana na ombi la spika kuwa wakati umefika wa kuienzi Kongwa hata kama ni kwa kuwa na jengo ambalo litakumbusha haya au uwanja wa ndege alioutumia Rais wa Misri na Algeria na nitakapokutana na marais hawa nitawaeleza kwamba kuna uwanja waliutumia viongozi wenu lakini bado haupo vizuri, nitachomekea chomekea,” amesema Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment