Wednesday, July 31, 2019

WAZIRI MKUU ATAKA MKANDARASI KUTUMIA VIBARUA WA NDANI YA HALMASHAURI

Na Hadija Hassan, Lindi.

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amemuagiza Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi, M/S National Service Construction Department (SUMA JKT ) kutotumia vibarua wanaotoka nje ya Wilaya hiyo na Badala yake wawatumie Vijana waliopo katika Halmashauri hiyo.


Majaliwa aliitaka agizo hilo kwa Meja Atupele Mwamfupe Jana baada ya kutembelea na kukagua eneo linalojengwa Ofisi hiyo ambapo alisema kuwa katika eneo hilo wapo Vijana wa kutosha wa watakaoweza Kufanya Kazi kwa uweledi katika ujenzi huo.


Hata hivyo Majaliwa alisema ili kuifanya Kazi hiyo iende kwa kasi na kukamilika katika muda uliopangwa Ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za kuwatoa vibarua nje ya Maeneo hayo ni vyema kutumia vibalua waliopo ndani ya Wilaya hiyo.


Awali akisoma taarifa ya Mradi huo Mbele ya Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ya Ruangwa, Andrew Chezue alisema kuwa Mradi huo utagharimu Tsh. Bilioni 3,777,831,596.00 na unasimamiwa na Mtaalamu Mshauri M/S Bureau for Industrial Cooperation (BICO) kwa Mkataba wa Tsh. Milioni 16,205,000.00


Chezue alisema mradi huo umeanza rasmi mwezi Juni Mwaka huu wa 2019, na unatarajiwa kukamilika mwezi juni Mwaka 2020 ambapo lengo lake kubwa ni kuboresha mazingira ya kufanyia Kazi ikiwa pamoja na kuwa na jengo bora na imara ambalo litatumika katika Shughuli Mbali mbali za Kiserikali.


Hata hivyo Chezue alibainisha kuwa Mpaka sasa jumla ya Tsh. Milioni 500,000,000.00 zimeshatolewa na Serikali kuu kwa Mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambazo zimetumika kwa kumlipa Mkandarasi kwa ajili ya malipo ya awali (Advance payment), ili aweze Kufanya stadi ya udongo pamoja na kusafisha eneo la mradi.


Nae Meneja wa Kanda ya ujenzi wa Suma Jkt Kanda ya kusini, anaetekeleza mradi huo wa ujenzi wa Ofisi Mpya ya Halmashauri, Meja Atupele Mwamfupe alisema kuwa jengo hilo Litakuwa la ghorofa Moja ambalo  litahusisha vyumba 33 Chini na vyumba 29 Juu pamoja na kumbi mbili za mikutano.


Alisema mpaka sasa Kazi zilizokamilika ni pamoja na usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi, upimaji wa sampuli ya udongo, uchimbaji wa kisima cha maji, ukusanyaji wa Vifaa vya ujenzi eneo la Mradi, ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la Mradi pamoja na ufyatuaji wa matofali ambao unaendelea ambapo hadi sasa tofali 10,000 zimeshafyatuliwa.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Rashidi Nakumbya aliishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuipatia Halmashauri hiyo fedha za ujenzi wa Ofisi Mpya na ya kisasa Itakayokuwa na mchango Mkubwa katika kuongeza ufanisi wa Kazi kwa watumishi wa Halmashauri hiyo.


NaKumbya aliongeza kuwa Kutokuwa na Ofisi kubwa katika Halmashauri hiyo hivi sasa kunasababisha mtawanyiko wa baadhi ya Idara kunakotokana na ukosefu wa majengo hali ambayo wananchi hupata shida wanapokwenda kupata huduma.


Hata hivyo alieleza changamoto nyingine kuwa ni kuwepo kwa Msongamano wa watumishi kutumia Chumba kimoja baina ya Wakuu wa Idara na vitengo katika Idara jambo ambalo linapelekea kupunguza ufanisi wa kazi.

Utayarishaji wa eneo la ujenzi ukiwa unaendelea.
 
 Muonekano wa Jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi litakapokamilika.

PICHA ZOTE NA HADIJA HASSAN. 

No comments:

Post a Comment