Sunday, July 28, 2019

MGALU AWATAKA TANESCO KUPELEKA FOMU RUHARUKE

Image may contain: Subira Mgalu, smiling, standing and closeup
Na Omary Mngindo, Rufiji.

NAIBU Waziri wa Nishati Subira Mgalu amewataka maofisa wa Shirika la Umeme nchini Tanesco, kufika katika kijiji cha Nyamtimba Kata ya Ruharuke wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuwapelekea fomu za maombi ya umeme wananchi wa eneo hilo.


Sanjali na hilo Naibu Waziri huyo amewataka maofisa hao kuwapatia elimu wananchi, ili wasijikute wanaangukia katika mtego wa watu wanaojitambulisha ni watumishi wa shirika (vishoka), wanajitangaza ni maofisa, hivyo kuwachukulia fedha pasipokuwa na utaratibu.


Mgalu ametoa kauli hiyo kijijini hapo, baada ya mkazi Ally Monero kusema kuwa wanatozwa sh. 40,000, ambazo hazina risiti kwa ajili ya kutengenezewa miundombinu ya uwekwaji umeme kwenye nyumba zao, hali ambayo kwao imekuwa mtihani mkubwa.


"Naibu Waziri hapa kuna mkanganyiko wa gharama ya upatikanaji wa huduma ya umeme, tunasikia katika radio kwamba uunganishwaji wa umeme ni sh. 27,000, lakini cha kushangazwa tunatakiwa tutoe sh. 40,000 kwa ajili ya kutengenezewa miundombinu ya upokeaji wa huduma hiyo" alisema Monero.


Baada ya kauli hiyo ndipo Naibu Waziri Mgalu aliposimama na kuzungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo ufafanuzi wa malalamiko ya mkazi huyo ambapo amemuagiza Meneja wa shirika hilo Rufiji, kuwafuatilia watu hao wanaowatoza kiasi hicho cha fedha, kisha kuwachukulia hatua.


"Suala alilolielezea Mzee Monero la uwekwaji wa miundombinu ya upokeaji umeme, nakuomba Meneja wa Tanesco fuatilia hili la utozwaji wa fedha hizo ambazo hazikatiwi risiti, wataobainika wachukuliwe hatu kalia," alisema Mgalu.


Aliwataka watumishi wa shirika hilo kufika kijijini hapo kwa lengo la kuwapelekea fomu za maombi ya umeme, sanjali na elimu kuhusiana na utoaji wa elimu itakayowasaidia wasiangukie kwenye mikono ya watu wanaojitambulisha ni watumishi wa shirika kumbe sio.


Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Neema Omary alisema kuwa wanashindwa kuweka miundombinu ya umeme katika nyumba zao kutokana na kutoona hata nguzo katika naeneo ya nyumba zao, hali inayosababisha kutokuwa tayari kwa zoezi hilo.


Mbunge wa jimbo la Kibiti Ally Ungando aliwaambia wananchi hao kuwa serikali inaendelea na usambazaji wa umeme na miundombinu mingine kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaondokana na chaangamoto zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment