Wednesday, July 31, 2019

WANANCHI WA UDINDIVU, MAPINGA BAGAMOYO WATENGENEZA BARABARA KWA NGUVU ZAO.

Wananchi wa kitongoji cha Udindivu kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo wameiomba serikali kupitia Mamlaka ya usimamizi wa Barabara vijijini na mijjini (TARURA) kuwajengea makaravati katika ujenzi wa Barabara unaoendelea kwa nguvu zao wenyewe.


Wananchi hao wametoa ombi hilo baada ya kutengeneza barabara kwa kuchangishana wenyewe ambapo wamekwama sehemu zinazohitaji madaraja.


Wakiongea na BAGAMOYO KWANZA BLOG katika eneo hilo, wananchi hao wamesema kwa muda mrefu barabara hiyo imekuwa haipitiki kutokana na ubovu wake hali iliyopelekea wananchi kujikusanya kutengeneza wenyewe barabara hiyo.


Walisema barabara hiyo ilikuwa imejaa mashimo, na kipindi cha mvua hujaa maji na kupelekea wananchi kushindwa kabisa kuitumia barabara hiyo.


Waliongeza kuwa, hapo awali gari zilikiwa haziwezi kupita hivyo hata kusafirisha wagonjwa kuwafikisha zahanati ilikuwa ni shida kutokana na hali ya barabara hiyo.


Barabara hiyo ni kiunganishi kati ya kata ya Mbweni jijini Dar es Salaam na kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo ambayo husaidia wananchi katika shughuli zao za kila siku.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Udindivu, Chandika Dismas alisema ujenzi huo wa barabara unagharimu shilingi milioni saba ikiwa ni michango ya wananchi.


Alisema wananchi wenyewe waliamua kuunda umoja wao ili kutengeneza barabara hiyo ambapo bajeti yake ni shilingi milioni saba na kwamba kazi inaendelea vizuri kutokana na wananchi wote wamekubaliana kwa kauli moja kuitengeneza kwa manufaa yao.


Aliongeza kuwa, pamoja na kazi hiyo kubwa iliyofanywa na wananchi, bado kunahitajika madaraja ambayo yapo nje ya uwezo wa wananchi na kwamba tayari wamewasiliana na Halmashauri ya Bagamoyo li waweze kuwasaidia sehemu zinazohitaji madaraja.

 
Kaimu meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa Barabara vijijini na mijjini (TARURA) wilaya ya Bagamoyo,Mhandisi Christopher Philip alisema wanatarajia kuiweka kwenye bajeti ijayo ili kuwaondolea adha wananchi wa Kitongoji hicho.

Wananchi wa kitongoji cha Udindivu kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo, wakiendelea na kazi ya kutengeneza barabara katika kitongoji hicho.
Wananchi wa kitongoji cha Udindivu kata ya Mapinga wilayani Bagamoyo, wakiendelea na kazi ya kutengeneza barabara katika kitongoji hicho.

No comments:

Post a Comment