Monday, July 29, 2019

MHANDISI KILUMBI AMSHUKURU DKT. MAGUFULI

Na Omary Mngindo, Kibuta.

DIWANI wa Kata ya Kibuta wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Mhandisi Juma Kilumbi, ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli, kwa kuipatia Kata yake sh. Mil. 93,200 zilizotumika kujenga madarasa katani humo.


Sanjali na hilo pia amemshukuru Waziri Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo ambaye ni mbunge wa jimbo hilo kupitia mfuko wa jimbo kwa kuipatia Kata sh. Mil. 2, kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.


Aidha vijiji vya Mlegele na Mloo ndani ya Kata hiyo vimepatiwa fedha za ujenzi wa vyumna vya madarasa na matundu ya vyoo kwenye shule hizo, hatua inayolenga kuboresha sekta hiyo wilayani Kisarawe.


Kilumbi alisema kuwa Mlegele imepatiwa sh. Mil. 40.6 sanjali na shule ya Kijiji cha Mloo, ambazo zote zimepelekewa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule katika vijiji hivyo, ambavyo vyumba vyao vilikuwa katika hali mbaya ya kuendelea na utoaji wa elimu.


"Pia tumepokea sh. Mil. 294 kwa ajili ya uwekaji wa miundombinu wezeshi shule ya sekondari ya Kata, ambayo mwakani itakuwa ya kidato cha tano na sita, zitajenga majengo mapya ya madarasa, mabweni, bwalo na vyoo, sanjali na ujenzi wa Maabara ambapo tumepatiwa sh. Mil. 12," alisema Mhandisi Kilumbi.


Aliongeza kuwa kupitia mradi mkubwa wa ujenzia reli ya Mwendokasi inayojengwa na Kampuni ya Yapi Markez, wamenufaika kwa uboreshaji wa elimu katani humo, huku akimshukuru Mkuu wa wilaya hiyo Joketi Mwegelo, kwa kasi yake inayolenga kutokomeza ziro wilayani humo.


"Katika wilaya yetu kuna ushirikiano mkubwa kuanzia viongozi wa vijiji, halmashauri ya wilaya pamoja na viongozi wa ngazi zote, umoja huu unaounganishwa na mbunge wetu Jafo ndio unaoleta maendeleo katika nyanja zote," alisema Kilumbi.


"Katika mpango wa serikali kusukuma juhudi za sekta ya elimu katani kwangu vijiji vya Kauzeni, Mlegele, Mtamba na Mloo vimenufaika na fedha kutoka serikali Kuu na mfuko wa jimbo, kwaniaba ya wana- Kibuta tunashukuru sana" alimalizia Kilumbi.

No comments:

Post a Comment