Thursday, July 11, 2019

SHULE WILAYANI RUANGWA ZABUNI MIRADI KUONGEZA KIPATO.

Na Hadija Hassan, LINDI.

Kutokana na Changamoto ya uchache wa fedha za Elimu Bure kutokidhi mahitaji Baadhi ya Shule za Msingi wilayani Ruangwa Mkoani Lindi zimebuni Miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuweza kujiongezea kipato.


Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Ng'ombe wa Maziwa katika Shule ya Msingi Matope na Mradi wa Shamba la Miembe ya muda mfupi katika Shule ya Msingi Chilangalile.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Walimu wakuu wa Shule hizo mbili , mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtope, Zunu Kigomba na Bakari Hamimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chilangalile, walisema kuwa kutokana na mahitaji waliyonayo katika shule zao fedha hizo zinazotolewa na Serikali haziendani na idadi ya wanafunzi waliokuwepo.


Nae Zuna kigomba alisema kuwa kutokana na Mradi wa Ngombe waliouanzisha baada ya kupata fedha za Elimu ya kujitegemea (EK) kutoka EQUIP T ulioghalimu Tsh. 15,000,000. umeweza kupunguza michango mbali mbali kutoka kwa wazazi kwa ajili ya kuandaa mitihani hasa kwa wanafunzi wa Darasa la Nne na Darasa la Saba.


“faida tuliyoipata kutoka katika huu Mradi tumekuwa tukipata fedha za kuchapa Mitihani bila kuhusisha fedha ya kapitesheni ya Shule, tumeweza kununua baskeli ya Shule , Sufuria kwa ajili ya kupikia chakula cha Wanafunzi, unatusaidia pia kununua vifaa vya kufundishia kama vile chaki na manila bila ya kukopa kopa maeneo Mengine "Alisema.


Aliongeza kuwa kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuendeshea shule kutotosheleza mahitaji wanalazimika kukopa kutoka Katika vyanzo vingine vya mapato ili kuendesha shughuli za Shuleni hapo.


Kwa upande wake Mratibu elimu Kata wa Kata ya Makanjiro Katherini Mbinga alisema kuwa Mradi wa miti ya Miembe ambapo pia umetokana na Mpango wa Elimu ya kujitegemea (EK) kupitia Mpango wa EQUIP T uliobuniwa katika Shule ya Msingi Chilangalile wenye gharama ya Tsh. 15,000,000, na Shule Zingine katika kata hiyo utaweza kuwasaidia katika utekelezaji wa Mikakati ya kuinua taaluma Ngazi ya Kata inayofanywa katika Halmashauri hiyo.


Alisema Mikakati mingi ya kupandisha ufaulu katika maeneo yao inakwama kutokana na changamoto ya kukosa fedha ya kutosha ya kutekeleza mikakati hiyo.


“tunapokaa na walimu kupanga namna ya kuinua taaluma lazima tuhitaji pesa, pesa ambayo mashuleni ukilinganisha fedha inayofika ni kidogo ambayo sisi kama ngazi ya kata kama ni kufanya mitihani, kufanya ziara za kimasomo, tunashindwa kutekeleza kwa sababu fedha haitoshi kwa hivyo kupitia huu mradi baada ya kuanza kuvuna mazao ni matarajio yangu shule hizi zitakuwa na kipato binafsi tofauti na ile fedha ambayo inaingia kutoka serikali kuu” 

  
Alifafanua Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chilangalile Bakari Amimu alisema kuwa Shamba hilo la Miembe Lina ukubwa wa Nusu hekta na lina miche 120 ambapo kila mche mmoja unatarajiwa kuzaa maembe 20 ambapo kwa mara ya kwanza wanataraji kuvuna maembe hayo ifikapo mwaka 2020.


Hata hiyo Abdull Nangomwa Ofisa Elimu Taaluma wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi akizungumza kwa Niaba ya Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo Alikili kuwepo kwa Miradi ya Maendeleo katika Baadhi ya Shule Wilayani hapo itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato ambayo itapelekea Kufanya ujazilizi katika fedha zinatoka Serikalini kwa ajili ya kufanya mambo mbali mbali katika Shule Zao

No comments:

Post a Comment