Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha ameitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini
kusimamia wabunifu kupata haki ya umiliki wa bunifu zao.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo
hilo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea mabanda ya Taasisi za Elimu
zilizo chini ya Wizara hiyo ambazo zimeshiriki maonesho ya 43 ya biashara ya
kimataifa maarufu kwa jina la Sabasaba na kukutana na mmoja wa wabunifu aliyeomba serikali imtambue kwa kuwa amebuni nyenzo ya
kufundishia mfumo wa sayari shuleni.
Alisema ni vizuri wabunifu
wanapoandaa kazi zao zikatambuliwa na kupatiwa haki miliki ya bunifu au
ugunduzi walioufanya lakini pia kuendelea kuwafadhili ili waweze kukuza bunifu
zao.
“Ninyi COSTECH hakikisheni bunifu
mbalimbali nilizoziona hapa sabasaba katika mabanda yetu haziishii katika
maonesho tu, bali zikuzwe na tumieni nafasi hii ya maonesho kuwakutanisha
wabunifu na wafanya biashara kwa ajili ya uzalishaji,” alisema Naibu Waziri Ole
Nasha.
Katika hatua nyingine Waziri Ole
Nasha ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kazi
nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kukuza ubunifu na ujuzi na kuwataka
kuendelea kusimamia bunifu mbalimbali za wanafunzi ili ziingie katika soko na
kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizoshiriki maonesho ya Sabasaba kwa mwaka 2019
ni pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Afya
na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo
Kikuu Mzumbe, Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Tume ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Chuo Kikuu cha Sayansi
na Teknolojia Mbeya (MUST)
No comments:
Post a Comment