Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akikagua moja ya kituo cha kuchotea maji cha
Mradi wa Maji Hedaru katika mji wa Hedaru, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
...................................
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb)
amekagua Mradi wa Maji Hedaru uliogahrimu Shilingi bilioni 1.7 kwenye Mji wa
Hedaru kwa lengo la kujionea changamoto zinazoukabili, ikiwemo usimamizi wa
mradi katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri Aweso amekagua vituo vyote vya maji
vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi katika mradi huo na kukuta
vyote vikitoa maji, lakini akabaini mambo yafuatayo:-
Chanzo cha maji kutokuwa na uwezo wa kukidhi
mahitaji ya wananchi.
Matumizi ya mfumo wa nishati ya jua badala ya
nishati ya umeme ambayo imefika kwenye mji huo.
Usimamizi mbovu wa Kamati
za Maji uliosababisha mradi kutojiendesha kwa faida.
Mgawanyo wa maji usio na uwiano sahihi na
kusababisha mgogoro kwa wananchi.
Mara baada ya kukagua mradi huo, Naibu Waziri Aweso
ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kusimamia
mradi huo katika kipindi cha mpito mpaka watakapo patikana viongozi wa kamati
mpya itakayosimamia mradi.
Pili, ameelekeza yafanyike mabadiliko ya mfumo wa
nishati ya jua kwenda kwenye umeme.
Tatu, ameelekeza kitafutwe chanzo kipya cha uhakika
kitakachokidhi mahitaji halisi ya wananchi.
Nne, amewataka wataalam kutoka Bonde
la Mto Pangani kufika na kutatua changamoto ya watumiaji maji.Tano, amesisitiza
ushirikishwaji na elimu itolewe kwa wananchi katika uendeshaji wa mradi ili
waweze kuwajibika katika maendeleo ya mradi.
Aidha, Naibu Waziri Aweso amesema kuna umuhimu
mkubwa wa kuwashirikisha wananchi katika hatua zote za ujenzi wa miradi yote ya
maji, waweze kuwa wasimamizi wazuri wa miradi itakayokuwa endelevu.
Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary
Senyamule wakati wakikagua Mradi wa Maji katika Wilaya ya Same, mkoani
Kilimanjaro.
Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa katika eneo lilipojengwa chanzo cha
Mradi wa Maji Hedaru katika Kijiji cha Gundusine, Wilaya ya Same, mkoani
Kilimanjaro.
Wananchi
wakichota maji katika kituo cha kuchotea maji cha Mradi wa Maji Hedaru katika
eneo la Hedaru B, wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwasikiliza wakazi wa Kijiji cha Gundusine
katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Tenki
jipya la kuhifadhi maji la Mradi wa Maji Hedaru, wilayani Same, mkoani
Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment