Kiwango cha ufaulu wa Darasa la saba
2017 kimeongezeka kwa asilimia 2.40 ukilinganisha na mwaka 2016.
Akitangaza matokeo ya darasa la saba
Katibu Mtendaji wa Baraza la mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Charles Msonde
alisema jumla ya watahiniwa 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani huo
wamefaulu kwa kupata alama 100 au zaidi kati ya alama 250 wanazopaswa kupata.
Dk Msonde amesema kati ya waliofaulu,
wasichana ni 341,020 ambao ni sawa na asilimia 70.93 na wavulana ni 321,015
sawa na asilimia 74.80 .
Amesema idadi ya watahiniwa waliofaulu
ni sawa na asilimia 72.76.
Dk Msonde amesema mwaka 2016 watahiniwa
waliofaulu walikuwa asilimia 70.36, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia
2.40.
Katibu Mtendaji huyo alisema ufaulu
katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hisabati umepanda kwa asilimia kati
ya 4.25 na asilimia 10.05 kulinganishwa na mwaka 2016.
"Kwa masomo ya Sayansi na maarifa
ya jamii ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 3.56 na asilimia 13.97
kulinganisha na mwaka 2016.
"Watahiniwa wamefaulu zaidi katika
somo la Kiswahili ambalo ufaulu ni asilimia 86.86 na somo walilofaulu kwa
kiwango cha chini zaidi ni Kiingereza, lenye ufaulu wa asilimia 40.30,"
amesema Dk Msonde.
Katibu Mtendaji, Dk Msonde amezitaja
shule 10 bora kitaifa kuwa ni St Peter iliyopo Kagera, St Severine
(Kagera), Alliance (Mwanza), Sir John (Tanga), Palikas (Shinyanga),
Mwanga (Kagera), Hazina (Dar es Salaam), St Anne Marie (Dar es Salaam),
Rweikiza (Kagera) na Martin Luther (Dodoma).
Amezitaja shule 10 ambazo hazikufanya
vizuri kuwa ni Nyahaa ya Singida, Bosha (Tanga), Ntalasha (Tabora), Kishangazi
(Tanga), Mntamba (Singida), Ikolo (Singida), Kamwala (Songwe), Kibutuka
(Lindi), Mkulumuzi (Tanga) na Kitwai A (Manyara).
Aliitaja mikoa iliyoongoza kitaifa kuwa
ni Dar es Salaam, Geita, Kagera, Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha, Mwanza,
Katavi na Tabora.
Dk Msonde amesema mikoa iliyofanya
vibaya ni Singida, Tanga, Tabora, Songwe, Lindi na Manyara.
No comments:
Post a Comment